Aliyoibua CAG kuhusu ARV yashughulikiwe

26Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyoibua CAG kuhusu ARV yashughulikiwe

SEHEMU ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebainisha kuwapo dawa zenye thamani ya Sh. bilioni 23.04 zilizokwisha muda wake katika maghala ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Ukaguzi huo uliofanywa mwaka wa fedha 2020/21 ripoti yake ilishakabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na Bunge kwa ajili ya kujadiliwa na wawakilishi wa wananchi, kwa mujibu wa sheria.

Alifafanua kuwa kiwango cha kwisha muda wa dawa kwa mwaka wa fedha 2020/21 kilikuwa asilimia tano ya gharama za mauzo ya Sh. bilioni 196.83 sawa na kiwango kilichoripotiwa mwaka 2019/20 cha asilimia tano.

Pia, kiwango hicho kilizidi kinachotakiwa kwa asilimia mbili kilivyoelezwa katika Aya ya 7.3.3 ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za MSD wa mwezi Juni 2018, huku MSD ikiwa na jumla ya bidhaa 7,676,436 za thamani ya Sh. bilioni 22.8 zilizopitwa na muda zilizokuwa kwenye maghala ya MSD kuanzia Aprili 16, 2000 hadi Juni 30, 2021.

Pia, CAG alibainisha kuwa MSD ilipokea fedha kutoka kwa wafadhili ambazo ni Dola za Marekani 239,023.92 ili kugharamia uteketezaji dawa za kupunguza makali ya VVU/UKIMWI, na kwamba licha ya ruhusa ya kuteketeza dawa hizo kutolewa na Wizara ya Fedha na Mipango tangu Oktoba 7, mwaka 2021, hazikuharibiwa hadi wakati wa ukaguzi mwezi Desemba 2021.

Aliendelea kueleza kuwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alibaini kuwapo ucheleweshaji wa kuomba vibali vya uhakiki wa vifaa tiba vya kuanzia mwaka 2014 hadi Juni 2020, ambavyo ni dawa, vifaa vya matumizi ya upasuaji na vitendanishi vilivopitwa na muda kutoka katika mamlaka za serikali zinazohusika.

Ripoti ya CAG imeibua tatizo hilo, hivyo ni vyema dawa hizo zilizoachwa zikaharibika, ziteketezwe ili kuepusha madhara mengine na pengine waliokuwa wanahitaji hawakupata kwa sababu ambazo hakuna anayejua.

Pia, ni muhimu kujua vifaa vilivyostahiki kuteketezwa viliachwa kuendelea kuwapo, licha ya kuwa ni hatari kwa afya na kwa mujibu wa sheria vinapaswa kuteketezwa.

Aidha, gharama ya kuhifadhi dawa na vifaa hivyo wakati zikisubiri kuteketezwa, zingeweza kutumika katika shughuli nyingine za kusaidia wananchi.

Tunatambua wapo Watanzania waliopo maeneo mbalimbali hasa ya vijijini wanatamani kupata dawa hizo, lakini huenda hawakuzipata inavyotakiwa, kwa sababu mbalimbali ambazo ni muhimu kujua ili walipakodi waweze kuelewa.
Yapo maswali mengi ya kujiuliza.

Kama nchi ina takwimu sahihi za mahitaji ya ARV maana yake inapoagiza au inapoomba msaada itaomba kwa kadiri ya mahitaji, ikiwa ni pamoja na kuweka makadirio ya watakaoongezeka kwa kuwa tayari takwimu za kuonyesha hali ya maambukizi na muda wanaotakiwa kuanza kutumia dawa hizo utajulikana.

Inapotokea dawa zinaharibika na hazijateketezwa inashangaza na kuzua maswali mengi, ndiyo maana tunaona kuna haja ya kila jambo linalozua maswali likajibiwa.

Tayari CAG amebainisha hatari iliyopo kwa wafanyakazi wa maghala yaliyohifadhi dawa hizo, jambo ambalo sio sawa.

Tunaamini penye wengi kuna mengi hasa ya watu kutaka kujitafutia fedha kwa njia haramu.

Ni muhimu ukafanyika uchunguzi kabla ya kuteketeza kujiridhisha kuwa kiwango kilichohifadhiwa ndicho kilichopo hadi siku ya uteketezaji, na kama kimepungua ni muhimu kujua zilikwenda wapi na waliofanya hivyo wachukuliwe hatua.