Kongole TRA kwa kutoa msamaha huu

27Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kongole TRA kwa kutoa msamaha huu

JUZI Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza msamaha wa adhabu na riba ya kodi kwa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha vikiwamo vilivyoingizwa kwa njia zisizo rasmi.

Pia, vilivyokusudiwa kwenda nchi jirani na vikaingizwa nchini kinyume cha taratibu  vilivyoingizwa nchini kwa muda na kuzidisha muda wa kukaa nchini na vilivyotumia msamaha wa kodi kinyume cha sheria au kubadilisha umiliki bila kufuata utaratibu.

TRA ilisema msamaha huo unatolewa kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 70 kifungu kidogo cha pili cha sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria ya fedha ya mwaka 2021 pamoja na kifungu cha 249 cha sheria ya usimamizi wa uhuru wa forodha ya Jumuiya Afrika Mashariki ya 2004 ambazo zinampa kamishna wa TRA mamlaka ya kusamehe riba na adhabu.

Aidha, ilibainisha kuwa msamaha huo unatolewa kuanzia jana hadi Juni 30, mwaka huu, ukiwa na lengo la kutoa unafuu kwa wamiliki wa vyombo vya moto vyenye madeni ya kodi na adhabu, ili kulipa kodi waliyokadiriwa tu bila adhabu na riba.

Mamlaka hiyo ilisema msamaha huo umelenga kujenga ushirikiano na uhusiano mwema kati ya TRA na walipakodi husika, kuwapa motisha ya kulipa kodi kwa hiari na wakati pamoja na kuweka kumbukumbu au taarifa sahihi za umiliki wa vyombo hivyo.

Tunaipongeza TRA kwa hatua hii kwa kuwa tunaamini inakwenda kuleta mabadiliko na kwamba yenyewe itapata kodi yake ambayo itaelekezwa kwenye utekelezaji wa shughuli mbalimbali za serikali.

Lakini itapunguza au kuondoa kabisa msongamano wa magari yaliyokuwa yamekamatwa kwenye maeneo mbalimbali ya bandari, maana yake hata wenye jukumu ya kulinda watapunguziwa mzigo kwa kiasi kikubwa.

Tunaamini utasaidia wananchi kupata vyombo vyao vya usafiri ambavyo watavitumia nchini au nchi walizokuwa wanapeleka, maana yake yalibaki na huenda mengine yaliharibika au kutolewa vifaa kabla ya kuwafikia wahusika.

Tunawasihi wafanyabiashara na wote waliokwama kutoa magari yao kwa sababu ya riba na adhabu mbalimbali,kutumia vyema muda uliotolewa kwa kuchukua mali zao kuliko kuacha kabisa kwa kuwa ndiyo wakati mwafaka.

Hii ni motisha nzuri inayopaswa kuigwa,kwa kuwa ili nchi iendelee inahitaji kodi na lazima ipatikane kutoka kwa wananchi wa nchi yake,pale ambako inaonekana kuna linaloweza kufanyika kurahisisha kodi kulipwa ni jambo jema kama TRA walivyofanya.

Tunaisihi TRA kuangalia maeneo mengine ambayo wanaweza kukusanya kodi ya serikali kwa urahisi kwa kutoa motisha kama walivyofanya kwa wenye magari haya.

Lakini elimu kwa walipa kodi na kujenga mazingira rafiki ili walipe kodi halisia kwa hiyari ni muhimu sana,kwa maendeleo ya nchi,kwa kuwa tunaamini wanaolipa kwa hiyari ni wenye kuipenda nchi yao.

Tunaamini wananchi wakielimishwa na kuona kodi zao zinatumika vizuri na kwamba zinaleta mabadiliko kwenye maisha yao,watalipa kwa hiyari na watafurahia kulipa.

Nchi zilizoendelea mtu kukwepa kodi ni kosa kubwa la jinai, na hatua kubwa huchukuliwa haraka kwa wahusika bila kujali umaarufu wala nafasi ya mhusika katika jamii.

Kwa nchi za Afrika,wakati mwingine ni kawaida kusikia mfanyabiashara au mtu maarufu fulani amekwepa kodi, na bado asijitokeze mbele ya umma kuonyesha anajutia na kulipa fedha ya umma.

Ni lazima kujenga nidhamu ya watu kuipenda nchi yao na kuona kulipa kodi ni jukumu la lazima kwake,hapaswi kukwepa kwa namna yoyote bali ajitokeza mbele ya umma kujisifu alivyolipa kodi nzuri kwa nchi yake.

Naamini kila Mtanzania akilipa kodi kwa hiyari tutakuwa na fedha nyingi ambazo zikielekezwa kwenye matumizi sahihi ya kuhudumia wananchi kwenye mambo yanayowagusa moja kwa moja,zitasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ya nchi.

Mwananchi anataka kuona namna kodi yake inatumika,kwamba anaposikia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),kuna mabilioni yametumika vibaya inakatisha tamaa, hivyo tunashauri serikali kuziba mianya yote yenye kupoteza mapato ili ziende kwenye njia sahihi.