Ofisi ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imewatangazia wananchi na taasisi mbalimbali kwenda kwenye mikutano ya hadhara na ya ndani kuwasilisha maoni yao.
Maoni yanalenga katiba, uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu, umoja wa kitaifa, ushiriki wa wanawake na makundi maalum katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
Mengine ni elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma.
Katika tangazo hilo wametaja eneo la mkutano huo kuwa ni ukumbi wa Adam Sapi wa ofisi ndogo ya Bunge mkoani Dar es Salaam na kikosi kinaanza kukutana na wadau kupokea maoni na mapendekezo yao.
Wadau wakiwamo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba (JUKATA) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) ni miongoni mwa wanaotajwa.
Wengine ni pamoja na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kanisa la Sabato Tanzania, Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) na wengine wengi.
Wakati kikosi kazi hiki kinakwenda kuanza jukumu hilo, Watanzania hawajasahau kazi iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ambayo iliwafikia wananchi mbalimbali kupokea maoni yao na kuandaa rasmu ya katiba.
Andiko hilo lilifikishwa kwenye Bunge la Katiba, lakini mchakato haukuwaletea katiba mpya, huku kundi moja likisusia licha ya baadaye ilipatikana Katiba Inayopendekezwa ambayo baadhi ya watu waliifananisha na kivuli cha katiba ya mwaka 1977 inayotumika leo.
Ni ushauri wetu kwa kikosi kazi kuwafikia wadau wote ili kujua kile wanachokitaka.
Tukumbuke wakati wa Tume ya Jaji Warioba wakifanya mikutano na wananchi vijijini ambao walieleza wanataka katiba ibebe nini kwa kuwa ndiyo muongozo wa maisha ya Watanzania.
Pamoja na kukutana na baadhi za taasisi zikiwamo za kidini tunashauri kuhakikisha wananchi wengi wanafikiwa ili maoni au mapendekezo yatakayofikishwa kwa Rais Samia, yawe yamekibeba kile Watanzania wanachotaka kifanyike ili kuwa na uwanja sawa kudumisha demokrasia, kuleta maendeleo ya uchumi ya raia na taifa.
Ni ushauri wetu kwa kikosi kutengeneza mfumo wa kupokea maoni kwa mtandao ili kuwe na uwanja mpana wa watu wengi zaidi kutoa maoni yao, ili wanapokuja kuandika ripoti isheheni mawazo na maoni ya wengi.
Tunaamini kuwa kwa kutumia teknolojia kazi ya kuchukua maoni itakuwa siyo ya gharama kubwa kwa vile wakati mwingine, hakutakuwa na ulazima wa kusafiri kwenda maeneo mbalimbali kwa vile itawezesha kuwafikia wananchi wengi zaidi ambao wataeleza kile wanachoona kinafaa kwa njia ya kielektroniki.
Kuwapo kwa watu wengi na maoni mengi kutaondoa hisia kuwa wajumbe walikwenda kukusanya maoni wakiwa na ripoti au majibu waliyotayarisha kabla.
Tunaamini ushirikishwaji mkubwa wa sauti za umma ipasavyo kile kitakachofikishwa kwa Rais na baadaye kufanyiwa maamuzi kitakuwa na tija kwa maisha ya kila Mtanzania.
Katka dunia ya sasa yenye ukuaji wa demokrasia watu wana hiari ya kuchagua wanachoona kinawafaa, lakini ni wakati ambao kuna vyama vingi ambavyo ni uamuzi binafsi kuwa mfuasi wa chama fulani na kwa kuwa moja ya kazi ya kikosi hicho ni kuangalia demokrasia ya vyama vingi ni muhimu wakafanya kazi yao kwa misingi ya haki na weledi na kuepuka kutaka kuwaridhisha watawala.
Tunaamini wakipata sauti sahihi na za wengi watamfikishia Rais ujumbe wenye uhalisia ili kuwezesha kufanya maamuzi, kwa kuwa ndani yake kuna mambo makubwa na magumu kama la katiba mpya, ambalo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alilianzisha lakini halijafanikiwa.