Serikali isikilize kilio cha waagizaji magari

20Apr 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali isikilize kilio cha waagizaji magari

HIVI Karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam, alisema magari yaliyotengenezwa chini ya mwaka 2010 yasiingizwe nchini, ili kuepusha nchi kuwa dampo.

Agizo hilo liliwaibua waagizaji na wauzaji wa magari wakiomba serikali ipunguze ushuru, ili Watanzania wengi wenye kipato cha kawaida waweze kuyaagiza matoleo mapya.

Wauzaji hao walisema wateja wao wamekuwa wakiagiza matoleo ya zamani kwa sababu ya bei zake kuwa chini, ambayo wana uwezo wa kuimudu ikilinganishwa na matoleo mapya.

Mathalani, Kampuni ya Jan International Limited inayojishughulisha na uuzaji magari ilisema asilimia kubwa ya wateja  hununua magari ya mwaka 2005, 2006 na 2008 kutokana na bei yake kuwa chini.

Alitolea mfano kwa wanunuzi wa magari madogo yaliyotengenezwa mwaka 2010 kushuka chini bei zake huwa ndogo, ambazo huanzia Sh. milioni 15 kulingana na aina ya gari.

Kampuni ya SBT Japan ofisi ya Tanzania, ilisema kwamba mteja anapokwenda kwao na kuchagua gari ya toleo la zamani siyo kwamba analipenda zaidi bali ni kutokana na thamani yake sokoni.

Alitolea mfano mteja anataka kuagiza RAV4 ya mwaka 2012 thamani ya kununua gari hilo nchini Japan ni kubwa na ushuru kwa makisio mteja anatakiwa awe na fedha siyo chini ya milioni 40.

Kwamba RAV 4 toleo la zamani mfano ya 2004 unaweza kutumia Sh. milioni 25 wakati toleo la sasa kuagiza peke yake unaweza kutumia siyo chini ya milioni 20.

Meneja wake alisema siyo kwa watumishi wala wafanyabiashara kwenye asilimia 100 labda wanaoagiza magari ya toleo la sasa ni asilimia tano.  Endapo itakuwa hivyo kama walivyoelekeza kwa sababu bado kauli yake haijatolewa ufafanuzi kama yazuiwe kabisa ya chini ya mwaka 2010 au ni mkakati upi utawekwa.

Wauzaji na waagizaji hao wanapendekeza serikali kupunguza kodi, ili kuwezesha wengi kuagiza magari ya kisasa ambayo wanaweza kuyalipia kwa kuwa bei ya kununua huwa ni chini zaidi ya ushuru unaotakiwa kulipwa.

Nipashe tunakubaliana na kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha nchi yetu haigeuzwi kuwa dampo la bidhaa chakavu, bali tupate mpya, lakini changamoto kubwa ni uwezo wa wananchi wengi kununua kipya na kumudu kodi inayotakiwa.

Watu wengi wanapambana kuwa na magari binafsi kutokana na kwamba usafiri wa umma, bado haujafikia viwango vinavyotakiwa kwa maana ya kwamba mtu anaweza kupanda daladala au hiace akaenda kazini na kurudi kwa urahisi zaidi.

Kama hali ingekuwa hivyo, basi wengi wangeridhika na kuutumia usafiri wa umma katika shughuli zao nyingi, na wengine kutoona ulazima wa kununua magari.

Ili kufikia malengo ni muhimu kuboresha usafiri wa umma, mathalani ujio wa mwendokasi Dar es Salaam walitarajia kila njia yanapopita kutakuwa na ahueni ya usafiri; kwamba mtu ataweza kuegesha gari na kupanda usafiri huo, ili kupunguza magari madogo kuingia katikati ya mji.

Kwa sasa mafuta yamepanda bei kiasi cha wengi kutamani kuegesha magari, lakini wanashindwa kutokana na ubora wa usafiri huo.

Tunatambua jambo hili ni la kisheria, lakini ni muhumu kuangalia hali ya maisha ya watu kwa kuwasaidia wananchi kununua magari kwa ajili ya kuwa na uhakika wa usafiri, na kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kuwa na magari chakavu.

Nia njema ya serikali kuzuia nchi iwe dampo kwa magari, iende hadi kwenye bidhaa nyingine kama za umeme, nguo, viatu na ujenzi ambazo husababisha wananchi kupata hasara, au fedha zao kutumika kwa manunuzi ambayo hayawezeshi maisha yao kubadilika.