Uhuru wa vyombo vya habari sasa uheshimiwe

04May 2016
Mhariri
Nipashe
Uhuru wa vyombo vya habari sasa uheshimiwe

JANA Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani.

Kabla na kilele cha maadhimisho hayo, wanahabari na wadau wa habari katika maeneo mbalimbali nchini walikutana kupitia semina, mikutano, makongamano na warsha kujadili mambo mbalimbali yanayohusiana na uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Kupitia mikusanyiko hiyo, mambo kadhaa yalijadiliwa, vikiwamo vikwazo vinavyokwaza uhuru wa habari nchini.

Wadau wa habari mkoani Morogoro wameadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa kufikisha kilio chao wakiitaka serikali kurekebisha na kuzifuta sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari.

Wadau hao waliwasilisha ujumbe huo katika maandamano waliyoyafanya kwenye mitaa mbalimbali ya mji wa Morogoro, wakiwa na mabango yenye ujumbe huo.

Walilaani vitendo vya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari kutowatendea haki waandishi wa habari pamoja na kuendelea kuwapo kwa sheria kandamizi

Kwa ujumla, wanahabari na wadau wa habari waliendelea kupaza sauti kama wafanyavyo kila mwaka wakati wa kuadhimisha siku hiyo, wakisema kuwa sheria kandamizi zinapaswa kufutwa na kumtaka waziri mwenye dhamana ya habari kusikiliza kilio chao na kulipatia suala hilo ufumbuzi.

Walieleza kwamba, kilio hicho ni cha muda mrefu lakini kutokana na kutokuwapo kwa chombo imara kinachoweza kusimamia mambo ya habari, uhuru wa vyombo vya habari hauwezi kuwa na maana ikiwamo maslahi ya waandishi wa habari.

Mathalani, wanahabari, wadau wa habari na makundi kadhaa ya jamii nchini wamekuwa wakilalamikia uwapo wa sheria kandamizi ambazo ni kikwazo kwa uhuru wa habari nchini. Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970.

Kwa mfano, Sheria ya Magazeti imekuwa ikilalamikiwa kutokana na kumpa mamlaka waziri mwenye dhamana ya habari kulifunga gazeti wakati wowote anapotaka bila kulazimishwa kutoa taarifa kwa chombo husika wala kutoa fursa ya kujitetea.

Tume kadhaa ikiwamo ya Jaji Nyalali ziliwahi kupendekeza kwamba sheria hizo na nyingine kadhaa zimepitwa na wakati, hivyo zifutwe, lakini serikali hadi leo hii imeendelea kuzitumia.

Matumizi ya sheria hiyo yanaifanya serikali kuwa ndiye mlalamikaji, polisi, mwendesha mashtaka na hakimu, hali inayopora mamlaka ya mihimili mingine kama wa mahakama. Itakumbukwa kwamba mahakama imepewa mamlaka kikatiba kusikikliza mashauri na kuyatolea maamuzi.

Kutokana na utata huu, ni wakati mwafaka kwa serikali kupeleka mahakamani mashauri yoyote yanayokusu vyombo vya habari ili mhimili huo uyasikilize na kuyatolea maamuzi.

Kadhalika, serikali inaweza kulalamikia chombo chochote cha habari katika vyombo vya wanahabari kama Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Vile vile, kumekuwapo na mvutano kati ya wanahabari, wadau wa habari na serikali kuhusu muswada wa habari. Kwa upande wake, serikali ilitaka kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Vyombo vya habari na Muswada wa Haki ya Kupata Taarifa wa mwaka 2015, huku wanahabari na wadau wa habari wakipinga hatua hiyo, wakidai kuwa wadau hawakushirikishwa, hivyo serikali kuundoa miswada hiyo bungeni kufuatia ushauri wa aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda.

Tunashauri mchakato wa kupata sheria hii uharakishwe na ikiwezekana uwe mwaka huu, lakini la msingi wadau washirikishwe kutoa maoni yao kwanza na yazingatiwe.