Wauguzi, madaktari hospitali zetu za umma waache unyama kwa wagonjwa

05May 2016
Mhariri
Nipashe
Wauguzi, madaktari hospitali zetu za umma waache unyama kwa wagonjwa

KUNA matukio ambayo yamekuwa yakitokea mfululizo katika hospitali za umma, ya wauguzi kuwafanyia wagonjwa vitendo vya kinyama na kuwasababishia mateso makubwa.

Kuna matukio mengi, lakini kwa kutaja machache ni katika Hospitali ya Rufani ya Mbeya la Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, mapema wiki hii kufanya ziara ya kushtukiza na kumkuta mjamzito akilia mbele ya muuguzi aliyekuwa amekaa kwenye kiti akipiga soga bila kumhudumia. Muuguzi huyo alipoulizwa na Makalla kuhusu mjamzito huyo, alijibu kuwa atakuwa anaumwa uchungu na alianza kumhudumia baada ya Mkuu wa Mkoa kujitambulisha.

Makalla pia alimshuhudia mwanamke aliyelalamika kwake kuhusiana na tukio la kupigwa kofi na muuguzi mmoja alipokuwa anaumwa uchungu. Mwanamke huyo alimweleza kuwa alipigwa kofi la usoni na baada ya kujifungua alimchukua mtoto na kumbamiza kifuani kwake.

Kitendo cha mwanamke huyo kupigwa na muuguzi kilimkera Makalla na kumpa siku saba Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Godlove Mbwanji, kumchukulia hatua za kisheria muuguzi huyo na kusema kitendo hicho ni ukiukwaji wa maadili ya kazi na serikali haitavumilia kufanya kazi na watu wanaoifanya jamii ichukie.

Tukio lingine lilitokea jijini Dar es Salaam wiki iliyopita ambalo mganga wa zamu na wauguzi wawili wa Hospitali ya Amana wanadaiwa kuwa kutokana na uzembe walisababisha kifo cha dereva wa bodaboda, Nassoro Hamis (23), mkazi wa Ukonga, Mongo la Ndege. Kwamba Aprili 29, usiku vijana wawili walipempeleka mgonjwa wao hospitalini hapo kutokana na kupigwa risasi ya mguu na watu wanaosadikika kuwa majambazi, lakini wakakosa matibabu kwa sababu ya kukosa Sh. 20,000 zilizohitajika kwa mujibu wa wauguzi wa zamu.

Kutokana na malalamiko hayo, Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, amemwagiza Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Victoria Ludovick, kuwachukulia hatua za kinidhamu, mganga wa zamu na wauguzi wawili wa Hospitali ya Amana kwa uzembe uliosababisha kifo hicho.

Baada ya kupokea taarifa ya hospitali na maelezo ya ndugu wa marehemu, Meya huyo alisema tukio hilo lilisababishwa na uzembe.

Sababu kubwa ya kasi kubwa ya vitendo vya kinyama vinavyofanywa na wauguzi na baadhi ya waganga katika hospitali zetu za umma ni mmomonyoko wa maadili. Miongoni mwa mambo ambayo madaktari na wauguzi wanatakiwa kuzingatia ni kuwa na huruma kwa wagonjwa. Daktari au muuguzi anayekosa huruma kwa wagonjwa anakosa sifa na hafai kufanya kazi hiyo.

Vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi yao vinadhalilisha taaluma zao na pia vinasababisha hospitali kuonekana sehemu za mateso. Kibaya zaidi ni kwamba waathirika wakubwa wa unyama huo ni wajawazito, na hali hiyo ni hatari kwani kuna uwezekano mkubwa kwa mjamzito au mtoto aliyejifungua kupoteza maisha au wote wawili.

Tunawashauri viongozi wa serikali kuanzia wilaya, mikoa hadi taifa kujenga utamaduni wa kuzitembelea hospitali za umma zilizoko katika maeneo yao mara kwa mara na wakati mwingine kwa kushtukiza, kwani zinasaidia kubaini vitendo vya kinyama vinavyofanywa na wauguzi na waganga wasio na maadili ya taaluma zao na wasiowajali binadamu.

Tunashauri pia menejimenti za hospitali kuwafuatilia kw akaribu watumishi wao na wanaobainika kukiuka maadili wachukuliwe hatua, ikiwamo kufukuzwa kazi.
ends