Na Malinzi alitoa programu nzuri ya maendeleo ya vijana na kuanza kuendesha mashindano ya vijana kuanzia chini ya umri wa 13 ili kuhakikisha baadaye tunakuwa na timu nzuri za vijana kuanzia U-17 na U-20.
Lakini ukirudi kwenye msingi halisi wa uwekezaji kwenye soka ya vijana, Tanzania bado hatujafanya chochote, kwa sababu tunaanzia kuwekeza katika umri wa kati wa vijana na si umri mdogo.
Kitaalamu haswa tunapaswa kuwekeza kwenye soka ya vijana wa kuanzia umri wa chini ya miaka 10 na kuendelea, na hapo ndipo tunaweza kutemebea tukisema tumewekeza kwenye soka ya vijana.
Lakini pia kuna suala la walimu wa hao vijana wadogo, nalo ni tatizo kwa sababu makocha wengi wa vijana wadogo ni wale ambao wenye elimu na uzoefu mdogo ndiyo wanapewa jukumu la kupatia uzoefu na kujifunzia ukocha huko.
Ukweli ni kwamba vijana wadogo wanahitaji kufundishwa na makocha wa viwango vya juu vya elimu na waliobobea – tena inapendeza wakiwa ambao wana historia ya kufundisha watoto kwa mafanikio.
Kuanzia ngazi ya klabu na timu za taifa wamekuwa wakiletwa makocha wa viwango vya juu vya elimu na waliobobea kufundisha wachezaji wakubwa ambao tayari wamekosa msingi mzuri wa malezi ya kisoka.
Matokeo yake tunawapa kazi ngumu makocha wa kigeni, kwani wanapokutana na wachezaji wakubwa waliokosa msingi mzuri wa malezi ya kisoka, wanalazimika kuwapa mafunzo ya awali kabisa.
Na hali hiyo itaendelea iwapo tutaendelea kuleta walimu waliobobea kwa ajili ya kufundisha wachezaji wa kiwango cha Ligi Kuu, ambao hawajui hata kutuliza mpira wala kuomba au kutoa pasi.
Tunapaswa sasa kuleta makocha waliobobea kwa ajili ya kufundisha timu za vijana na pia kupiga hatua zaidi katika uwekezaji wa soka ya vijana, kuliko ilivyo sasa tunaanzia kwa vijana wa rika la kati badala ya wadogo kabisa.
Ndiyo maana leo Lete Raha tunasema, bila uwekezaji madhubuti kwenye soka ya vijana tutaendelea kusota.










