Uamuzi huo ulitangazwa na Rais Magufuli juzi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma na kueleza kuwa kodi hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 11 hadi tisa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya muda mrefu iliyokuwa ikitolewa mara kadhaa na Serikali ya Awamu ya Nne ya kushusha kiwango cha kodi ya mshahara kufikia tarakimu moja. Hata hivyo, hadi Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, anaondoka madarakani mwishoni mwa mwaka jana, ahadi yake hiyo hakuitekeleza.
Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuitekeleza ahadi hiyo kwa vitendo, tena mapema zaidi ikizingatiwa kuwa sherehe za Mei Mosi za juzi ni za kwanza kwake tangu aingie madarakani na kukuta changamoto nyingi, ukiwamo ukosefu wa fedha.
Kadhalika, hatua hiyo inaonyesha kuwa kiongozi huyo ana nia ya dhati ya kuwaboreshea wafanyakazi nchini mazingira ya kazi kutokana na kipindi hiki serikali yake kuelekeza nguvu zake katika kuweka sawa mambo mengi ambayo imekuta hayajakaa sawa.
Kufanya uamuzi huo ni jambo linalohitaji moyo kwa kuwa utaisababishia serikali kukosa fedha.
Pamoja na hatua hiyo ya serikali kuonyesha kwamba inawajali na kuwathamini wafanyakazi, punguzo hilo litawanufaisha zaidi wafanyakazi wenye mishahara isiyozidi Sh. 360,000 baada ya kukatwa fedha ya kuchangia mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa wanaopata mishahara zaidi hawataona unafuu mkubwa.
Katika hali hii, bado mfanyakazi hawezi kuona unafuu wa maisha kutokana na hali ya maisha kupanda kwa kasi kila uchao.
Sisi tunaona kwamba, pamoja na kupunguziwa kiwango cha PAYE, bado iko haja kwa serikali kuendelea kuangalia njia nyingine ya kuwaboreshea wafanyakazi mazingira ya kazi ili kwenda sambamba na hali halisi ya maisha.
Njia mbadala ya kuwapunguzia wafanyakazi hali ngumu ya maisha ni kuendelea kuboresha mishahara yao hususan wale wenye mishahara midogo. Jambo la kutia moyo ni ahadi ya Rais Magufuli juzi kwamba uchumi ukiendelea kuimarika, ataboresha pia mishahara ya watumishi.
Tunashauri kuwa, hatua hiyo ichukuliwe sambamba na mpango wa kupunguza mishahara ya vigogo katika baadhi ya mashirika ya umma, ikiwezekana mishahara itakayopunguzwa basi waongezewe watumishi wa ngazi ya chini.
Tunachukua fursa hii pia kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa uamuzi wake wa kuongeza kima cha chini cha mashahra kwa watumishi wa sekta ya umma kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 300,000 sawa na asilimia 100.
Ni uamuzi ambao umefanyika kwa wakati mwafaka kutokana na kilio cha muda mrefu kwa watumishi wa umma Tanzania Visiwani, ingawa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilikuwa ikiahidi kuwa itaongeza kima hicho baada ya uchumi kuimarika.
Ni matarajio yetu kwamba, waajiri katika sekta binafsi Tanzania Bara na Visiwani nao watauona umuhimu wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi wao na kuwaboreshea mishahara ili wakabiliane na ugumu wa maisha.










