Ubunifu, utekelezaji wa bajeti utaleta morali ya kodi

24Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ubunifu, utekelezaji wa bajeti utaleta morali ya kodi

BAJETI ya mwaka 2021/22 imepitishwa na Bunge kwa ajili ya kuanza utekelezaji kuanzia Julai mosi, mwaka huu, kwa kodi mpya kuanza kufanyakazi.

Akihitimisha mjadala wa mapendekezo ya bajeti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema walipakodi wakubwa ni 504, huku Watanzania walioandikishwa katika orodha ya walipakodi ni milioni 3.1.

Kwa mtazamo wetu, idadi ya walipakodi wakubwa ni ndogo na hii ni kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutafuta walipakodi wakubwa kwa uhalali.

Katika bajeti ya mwaka huu kuna ubunifu wa kutoza kodi ya majengo kwa kutumia luku za umeme, ambayo ufafanuzi wa serikali ni kuwa italiupwa na mmiliki wa nyumba na siyo mpangaji.

Huku ikielezwa nyumba za udongo za vijijini hazitatozwa kodi hii, kwa kuwa sheria ya majengo hairuhusu kufanyika kwa jambo hilo.

Licha ya ufafanuzi huu bado tunaona kusipokuwa na ufuatiliaji wa karibu wenye nyumba watalipa kwa kuwa ni watu gani watakwenda kukagua nyumba zilizofungiwa umeme kuwa ni za udongo au za tofali, lakini kuna nyumba za tofali lakini zimeezekwa kwa nyasi.

Pia, zipo nyumba zinatumia Luku zaidi ya moja kulingana na idadi ya wapangaji katika kuweka usawa wa uliopaji umeme kwa kadiri ya matumizi, maana yake nyumba moja italipiwa kodi hiyo zaidi ya mara moja.

Kadhalika, zipo nyumba za ‘Apartment’ ambazo hukaliwa na watu wengi na kila mmoja ana luku yake maana yake watalipa Sh. 5,000 kila mwezi.

Tunaunga mkono ubunifu wa kodi hii lakini ni lazima uwekwe utaratibu mzuri ili kuepuka kumkamua mwananchi wa kawaida kabisa.

Lakini kodi ya miamala na laini za simu nayo lazima iwekwe vizuri kwa kuwa bado watakaoumia ni wananchi wa kipato cha chini.

Tunashauri serikali kubuni vyanzo vipya zaidi vya mapato ambavyo havitawaumiza wananchi kwa kuwa wanalipa kodi kwenye bidhaa, mshahara na huduma nyingine wanazopata na sasa wanaletewa kodi nyingine ambayo itakatwa moja kwa moja.

Moja ya chanzo ambacho kinaweza kuleta fedha nyingi ni uchumi wa habari, na iliwahi kupendekezwa kwenye ripoti ya Chenge One ambayo iliona kuwa kuna uwezekano wa kupata mapato.

Wakati wa mjadala wa bajeti kilio kikubwa kilikuwa ni utekelezaji wa bajeti kutofikia lengo na sababu kubwa ni kuchelewa kutoka kwa fedha kama ilivyopangwa na kuchelewesha miradi ya maendeleo.

Jingine ni fedha kwenda kwenye matumizi ya kawaida kuliko kwenye miradi ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Tunataka kuona bajeti inatekeleza miradi ya maendeleo kikamilifu na isiwe bajeti ya matumizi ya mishahara, posho za vikao na madai mengine bali matumizi yanayogusa maisha ya mwananchi moja.

Maumivu ya kulipa kodi na tozo mbalimbali 22 zilizopitishwa na Bunge hayatakuwapo ikiwa mwananchi ataona kwenye eneo lake kuna huduma ya majisafi na salama, umeme, zahanati, kituo cha afya vyenye dawa na vifaa tiba, shule na barabara za kumwezesha kutoka eneo moja kwenda jingine.

Itapendeza mwezi kama huu wakati wa bajeti nyingine mwananchi asikie fedha za miradi ya maendeleo zilipelekwa zote na imetekelezwa kwa asilimia 100 na siyo utekelezaji chini ya asilimia 50, hii itaua morali ya kulipa kodi kwa mwananchi wa kawaida ambaye amebanwa moja kwa moja kupitia mifumo ya luku, laini za simu na miamala atakayofanya.