Aidha, Sh. bilioni 23 zimetolewa kulipa malimbikizo kwa watumishi 11,983 ikiwamo walimu.
Hii ni habari njema kwa watumishi ambao kwa muda mrefu walisubiri kupandishwa madaraja na kulipwa stahiki zao mbalimbali kwa mujibu wa sheria.
Tunaipongeza serikali kwa hatua hii, tunaamini morali ya kazi itaongezeka kwa kuwa kilio cha muda mrefu cha watumishi ni kulipwa stahiki zao muhimu kwa wakati, kiasi cha wengi kusota kwa muda mrefu katika daraja moja la kazi, na kila maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Mei Mosi, walipaza sauti zao kuhusu jambo hilo.
Rais Samia Suluhu Hassan amesikia kilio chao na sasa ametekeleza, jambo ambalo ni deni kwa watumishi kufanyakazi kwa bidii ili kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.
Katika hotuba zake zote Rais Samia amesisitiza uwajibikaji wa watumishi wa umma, ili kuhakikisha miradi na shughuli za serikali za kuwahudumia wananchi zinakamilika kikamilifu na kwa wakati.
Ipo miradi mingi ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, inahitaji usimamizi wa karibu na umakini wa watumishi wa umma ili kufikia lengo.
Miongoni mwao wapo watumishi wa sekta za afya ambao wana wajibu wa kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini, ikiwamo kuhakikisha hakuna wizi wa dawa na vifaa tiba vingine muhimu.
Pia, kwa walimu wanawajibu wa kufundisha kwa bidii ili kuongeza kiwango cha ufaulu na uelewa wa masomo kwa wanafunzi na kuwa na taifa bora la sasa na baadaye.
Watumishi wa umma watambue kuwa fedha wanayolipwa inatokana na kodi za Watanzania ambao wao wanapaswa kuwalipa kwa utumishi uliotukuka ambao unalengo la kutatua kero za wananchi wa kawaida.
Kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali ni kikubwa na sasa tunataka kuona uwajibikaji wenye tija na kuondokana na kufanyakazi kwa mazoea.
Wapo wanaosema kuwa uwajibikaji na kufanyakazi kwa bidii kupo sekta binafsi kutokana na ufuatiliaji wa karibu na ajira za mkataba hivyo mwajiriwa anapaswa kufanyakazi kwa bidii ili aongezewe mkataba na aendelee kuwapo kazini.
Wengi wanaamini wakishaingia serikalini ni ajira ya kudumu hadi atakapostaafu na wengi hufanyakazi watakavyo kwa maana ya kuzingatia muda wa kuingia na kutoka, lakini utendaji kazi bado siyo wenye tija.
Tunatarajia kuimarisha kwa mifumo ya ufuatiliaji utendaji kazi wa watumishi wa umma ili tija ya kodi ya Mtanzania ionekane kupitia kazi ambazo zitaleta matunda katika maisha ya wananchi.
Ikiwa kutakuwa na uwajibikaji hatutaona mabango, malalamiko mara viongozi wa kitaifa wanapofika kwenye maeneo yao kwa kuwa mambo mengi yatakuwa yametatuliwa.
Kama serikali inatimiza wajibu wake basi watumishi wahesabu ni deni kwao sasa ni wakati wa kuwajibika.










