Aidha, alisema gesi iliyogunduliwa nchi kavu na kina kirefu cha bahari ni futi za ujazo trilioni 57.54 mwaka 2021, ambao umewezesha kuanza kutumika kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati hususan kwa wazalishaji umeme, viwandani, majumbani na kwenye magari.
Wizara hiyo ilisema hadi Oktoba 2021 viwanda 52 mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Mtwara vinatumia gesi asilia, huku vituo vya kushindilia na kujaza nishati hiyo kwenye magari kwenye mikoa hiyo vikifanyakazi.
Pia imesema matumizi ya gesi asilia yamesaidia kupunguza utegemezi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu za maji, na hadi Novemba 2021 takribani asilimia 60 ya umeme unazalishwa kwa kutumia gesi.
Wizara hiyo inaongeza kuwa hadi Machi mwaka huu mapato yatokanayo na mauzo ya gesi yamechangia zaidi ya Sh. bilioni 208 katika mfuko wa mafuta na gesi kuanzia mwaka 2016/17 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, hadi Desemba mwaka jana, serikali ilipata mapato ya zaidi ya Sh. bilioni 441 yatokanayo na kodi mbalimbali kuanzia mwaka 2015 baada ya kukamilika kwa bomba hilo.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye takwimu, uhalisia ni kuwa asilimia 80 ya Watanzania bado wanategemea nishati ya mimea kwa ajili ya kupikia na shughuli nyingine.
Gesi ilipogundulika nchini ahadi ilikuwa ni kuisambaza kwenye makazi ya watu na wananchi wa Dar es Salaam, Mtwara na Lindi aliahidiwa kusambaziwa huduma hiyo nyumbani, ikiwa ni namna ya kupunguza bei ya nishati, lakini hali haikuwa hivyo.
Pia wananchi wa Mtwara na Lindi walipewa matumaini makubwa kuwa rasilimali hiyo inakwenda kubadilisha maisha yao kwa kuwa mikoa hiyo ingekuwa kama Ulaya au Dubai, kiasi cha kutokea vurugu kutokana na kuamini kuwa wanaporwa mali hiyo na walitaka ibaki huko kwa ajili ya kuwanufaisha wao kwanza kabla ya kuondoka.
Lakini hadi sasa hata wananchi wa mikoa hiyo hawajanufaika na nishati hiyo kwa matumizi ya nyumbani zaidi kwa kupata umeme kwa kuwa hawajaunganishwa kwenye gridi ya taifa.
Ikiwa gesi itawafikia wananchi wengi kwa bei rahisi maana yake watu wataachana na kukata kuni au miti kwa ajili ya mkaa, lakini kwa sasa kuna matumizi makubwa ya mkaa kwa kuwa bado mbadala uliopo haujatosheleza mahitaji.
Ni kweli serikali imeokoa fedha hizo ambazo zingenunua mafuta, lakini mzigo wa maisha uko kwa mwananchi wa kawaida, ambaye bado anatumia mkaa au gesi ya mitungi kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine, ambaye alitarajia kugundulika kwa gesi kungebadili maisha yake.
Katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya tabianchi yanaonekana dhahiri na dalili zikionekana kama jua kali, kipindi kirefu cha kiangazi ambacho husababisha ukame ambao huathiri binadamu, wanyama na viumbe wengine.
Kumekuwa na jitihada za kuhamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi, lakini kasi ya kuvuna mkaa ambao husafirishwa kwenda mijini ni kubwa ambako wengi hutumia gesi, mkaa na kuni. Kwa kawaida mti unaoteketezwa sasa ukipandwa mwingine itachukua miaka zaidi ya kumi kuuvuna, maana yake ni lazima kuwa na nishati mbadala na kuachana na kutegemea mimea.
Ni muhimu serikali ikatimiza azima yake ya kuhakikisha taasisi zote za umma hasa elimu na afya zinatumia gesi, ili kuondokana na matumizi ya kuni au mkaa ambayo ni uharibifu wa mazingira, vinginevyo nchi itabaki wazi na athari zitakuwa kubwa kwa wananchi.










