Tusifanyie mzaha maji

12Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tusifanyie mzaha maji

HIVI karibuni, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilitoa taarifa ya kuongezeka kwa joto na kuchelewa kwa mvua kutokana na jua la utosi, huku kukiwa na kasi ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, TMA ilitaja mikoa ambayo imekithiri kwa joto ni Kilimanjaro yenye nyuzi joto 36.4 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.6, Dar es Salaam nyuzi joto 33.8 ikiwa ni ongezeko la 2.2 na Ruvuma 34.

Siku chache baadaye Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), ilitangaza kuwapo kwa mgawo wa maji, na imeshatoa ratiba ya muda gani maji yatakuwa yanatoka sehemu gani.

Pia Mamkala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Moshi (MUWSA), ilisambaza ujumbe kwa wateja wake ikiwataka kutumia vizuri na kuhifadhi maji kwa kuwa yamepungua kwenye vyanzo vyake kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mgawo wa maji umeshaanza kama sehemu ya hatua za kukabiliana na tishio hilo, huku maeneo mengine yakikaa kwa takribani siku tatu hadi nne bila maji, na sasa biashara ya maji imerejea, ambapo walanguzi wanautumia mwanya huo kujipatia fedha.

Baadhi ya maeneo bei ni kati ya Sh. 200 na 500 kwa dumu, na wanaoumia ni wananchi wa kipato cha chini, ambao hawana vyombo vikubwa vya kuhifadhi maji kwa muda mrefu na sasa wanatakiwa kununua.

Juzi Waziri wa Maji, Juma Aweso, akizungumzia mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, alisema moja ya kero zinazoikabili mamlaka za maji ni upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa.

Alisema kiasi cha upotevu kinakadiriwa kuwa asilimia 20, na kwamba kiasi kikubwa kinapotea kutokana na wizi kwa kuwa kuna viwanda, nyumba za biashara na binafsi wameunganishiwa maji na hawalipi bili kwa mamlaka.

Licha ya wizara husika kueleza hasara wanayoipata kutokana na upotevu wa maji, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa na mamlaka hiyo kwa kuwa maji yanayopotea kwa kumwagika ovyo ni mengi sana.

Mathalani, ni kawaida kuona bomba la maji limepasuka na yanamwagika, mteja au mtu yeyote haruhusiwi kugusa na anapowajulisha wahusika huchukua hata siku mbili au tatu hadi wafike na kuziba.

Maji yanaendelea kumwagika kiwango ambacho kingejaza tangi la lita 2,000 au zaidi na kwa mwenye familia ya wastani angetumia kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Ni lazima mamlaka ziwekeze nguvu kudhibiti upotevu wa maji kwa kuvuja, ambayo mengi huishia ardhini na machache kuonekana juu ya ardhi, bila hivyo ni kuendelea kupata hasara ambayo ingeweza kuokolewa kwa kuboresha miundombinu na kuchukua hatua madhubuti.

Hali hii inatufundisha mambo mawili kwamba kama nchi tunatakiwa kuendelea na jitihada za kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji.

Ni muhimu kasi ya kuwafundisha wananchi umuhimu wa kuvuna na kutunza maji ya mvua ili yasaidie nyakati za kiangazi kama sasa, ingawa wengi hawafanyi hivyo.

Upo uwezekano wa kutunza maji mengi ya mvua, lakini bado nchi haijaweza kufanikisha hilo na sasa hali hii imekuja ili kukumbusha umuhimu wa kihifadhi maji kwa ajili ya nyakati zijazo.

Wananchi wanaoumia ni wa kipato cha chini kwa kuwa badala ya kutafuta fedha ya chakula, sasa wanatakiwa kununua maji ya kutosheleza mahitaji ya usafi wa mwili na nguo, pamoja na shughuli nyingine za nyumba. Lakini, lazima kuwe na elimu sahihi ya matumizi ya maji ili tuyatunze kwa ajili ya matumizi mengine.