Elimu ichangamkiwe Wiki Huduma Fedha

10Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Elimu ichangamkiwe Wiki Huduma Fedha

SERIKALI imeanzisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kitaifa ukiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21-2029/30 kupitia elimu ya umma ambayo ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa mpango huo.

Hivyo katika hatua za utekelezaji, Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa programu ya kutoa elimu ka umma ya mwaka 2021/22-2025/28. Programu imeweka mikakati ikiwamo matukio na mbinu zitakazotumika katika utoaji wa elimu ya fedha kwa umma.

Moja ya mikakati hiyo ni kuwapo kwa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kila mwaka ambapo elimu ya fedha itakuwa inatolewa kwa wananchi kupitia njia mbalimbali.

Katika utekelezaji wa programu ya utoaji elimu wa masuala ya fedha, serikali inakusudia ifikapo mwaka 2025 takribani asilimia 80 ya wananchi watakuwa wamepata uelewa wa masuala ya fedha, kutokana na utafiti kuonyesha kuwa uelewa bado ni mdogo.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa Finscope nchini wa mwaka 2017, ni asilimia 48.8 tu ya nguvu kazi ndio waliotumia huduma rasmi za fedha, hivyo kubaki na kundi la Watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizi, hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza Pato la Taifa.

Tunaona kwamba mkakati huu hususani wa kuanzishwa Wiki ya Huduma za Fedha ni njia yenye tija katika kufikisha elimu ya masuala ya fedha kwa kundi kubwa la Watanzania tukiamini kuwa itajenga uelewa na weledi katika matumizi sahihi ya huduma za fedha.

Pia itawezesha kuimarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia elimu ya fedha, kuongeza upatikanaji huduma za fedha, kutoa elimu ya kuwezesha kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha na kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha.

Kadhalika, itasaidia kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao, kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na kulipa madeni na kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Fedha kwenye ukuaji wa uchumi.

Kwa kuwa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yamefanyika kwa mara ya kwanza mkoani Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia Jumatatu hadi Novemba 14, tunawahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupata elimu ya masuala ya fedha ili wanufaike kiuchumi. Kwa kufanya hivyo, watapata uelewa wa masuala ya mikopo, uwekaji wa akiba, kuwekeza na matumizi sahihi ya fedha kutoka kwa watoaji wa elimu.

Ni matarajio yetu kuwa matokeo ya kuadhimishwa Wiki ya Huduma za Fedha yatakuwa chanya kwa watu binafsi, kaya, jamii na taifa kwa ujumla kwa kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha ufahamu elimu ya fedha na maarifa juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma rasmi za fedha.

Vilevile, kuimarika kwa matumizi ya masoko ya fedha, kusogeza huduma za fedha karibu zaidi na wananchi na kuhamasisha matumizi ya huduma hizo, kuwaunganisha wajasiriamali na fursa zinazotolewa na sekta ya fedha katika kukuza na kuimarisha biashara zao.

Elimu hii pia itawawezesha wananchi kupata maarifa na uelewa wa masuala ya fedha, hivyo kuwezesha kujenga utamaduni wa kutumia huduma rasmi za fedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.