BoT imechelewa kwa hili, lakini…

09Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
BoT imechelewa kwa hili, lakini…

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imetoa taarifa kwa umma kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria, baadhi ya wafanyakazi wa benki na taasisi za fedha wanaoshiriki ubadhirifu kupitia mikopo.

Aidha, ilibainisha matendo ovu ni kama rushwa wakati wa utoaji mikopo na kusababisha kuongezeka kwa mikopo chechefu na kutoza riba kubwa pamoja na kushirikiana na wakopaji kufanya udanganyifu.

Adhabu zilizotangazwa ni kuwafungia kuajiriwa na benki au taasisi yoyote ya fedha inayoendesha shughuli zake nchini, pia kwenye taasisi au benki inayosimamiwa na BoT.

BoT inasema utafiti uliofanywa unaonyesha ongezeko la mikopo chechefu katika sekta ya benki ni moja ya sababu kubwa ya benki na taasisi za fedha kutoza viwango vikubwa vya riba za mikopo na kuhatarisha uimara wa sekta hiyo na kuathiri uchumi wa nchi.

Katika kukabiliana na hilo, BoT imesema itaendelea kufanya ukaguzi wa benki na taasisi hizo ili kubaini sababu za kuongezeka kwa mikopo hiyo, na kwa wafanyakazi ambao watahusika moja kwa moja na mwajiri wake atatakiwa kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi yao.

Tunaipongeza BoT kwa hatua hii, licha ya kwamba imechelewa sana, lakini bado kuna nafasi ya kurekebisha kasoro zilizopo ambazo zilitokana na kutokuwapo ufuatiliaji wa karibu na kuchukua hatua madhubuti.

Baadhi ya wafanyakazi wa benki wamedaiwa kujihusisha na kuongeza mikopo au kukopa na wateja na baadaye kuwaacha hewani ambao wamejikuta wakilipa wenyewe na mwisho kugeuka kuwa mikopo chechefu.

Wapo ambao hushirikiana na wahalifu kwa kukopesha kampuni mikopo hewa na mwisho wanaopata hasara ni benki, lakini mtandao wa wanaofanya hivyo imekuwa ngumu kushughulikiwa na sasa tunaamini uamuzi wa BoT kuweka wazi utasaidia kupunguza au kumaliza.

Pia, imekuwa vigumu kwa wateja wa kawaida kuwafikia BoT na wengi kuishia kuumizwa na taasisi au benki husika.

Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa na utekelezaji wa agizo hilo ili kukuza sekta ya benki na kuleta mabadiliko makubwa yatakayosaidia ustawi na kupunguza au kuondoa maumivu kwa wananchi.

Miaka ya hivi karibuni kulikuwa na kasi ya benki na taasisi za fedha kuuza mali za walioshindwa kulipa mikopo, huku wengine wakichukua kadi za benki za wakopaji kwa ajili ya kutoa rejesho la mkopo kila mwezi.

Ukopeshaji huo umekuwa umiza kiasi cha wanaokopesha kunufaika na waliokopa kuwa na mzigo mzito na kushindwa kulipa madeni yao.

Unapokwenda kukopeshwa unakaribishwa kwa maelezo mengi mazuri na wakati mwingine kushawishiwa kuchukua mkopo mkubwa zaidi, huku ili upate fedha hizo unatakiwa kutoa rushwa kwa baadhi ya maofisa mikopo lakini bado utatakiwa kulipa pamoja na riba kubwa.

Hali hii ilikuwa ni maumivu na sasa uamuzi wa BoT kuingilia kati ni hatua muhimu katika kusaidia wananchi kutoumizwa na hata wanapoumizwa wachukue hatua gani au kwenda kwenye mamlaka gani.

Pia ni muhimu kuwa na elimu endelevu kwa wananchi ili wanapofanya maamuzi ya kukopa kwenye taasisi za fedha wanajua faida na hasara za kufanya hivyo, lakini kufuatilia kwa karibu na kutangaza hatua zinazochukuliwa.

Kwa sasa vikundi vya kijamii maarufu kama VICOBA vinavyotoa mikopo kwa wanakikundi vimepata nguvu kwa kuwa mtu anaona mkopo anaopata na riba yake ni nafuu, lakini hakuna rushwa wala mbinu chafu za kumuumiza, ingawa changamoto huwa ni pale wachache wanapoamua kukimbia na fedha husika.