Sababu kubwa za kiongozi huyo kuhoji ni kwa sababu bima ya afya inagusa Watanzania wengi hususan wa kipato cha chini, na kwamba ni muda mwafaka kwa muswada huo kufikishwa kwenye muhimili huo ili itungwe sheria.
Aidha, alisema ni muhimu serikali ikasema kama kuna mkwamo mahali ili Bunge lisaidie, baada ya kufafanua kuwa zimetengwa Sh. bilioni 149 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote.
Hoja hii inarudi tena bungeni kwa mara nyingine kwa kuwa wakati wa Mkutano wa Bunge wa Mei mwaka huu, yalipowasilishwa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wabunge walipaza sauti juu ya umuhimu wa bima ya afya kwa wananchi wote.
Aidha, walieleza namna wananchi wengi wanavyopata shida ikiwamo wengine kupoteza maisha kutokana na kutokuwa na bima ya afya, hivyo waliitaka serikali kuhakikisha inaupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Hakuna anayeweza kubisha kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa kila Mtanzania, ndiyo maana nchi zilizoendelea suala la bima ni lazima na kila mwananchi anayo kwa ajili ya kumwezesha kupata huduma bora za afya, hatua iliyoongeza muda wa kuishi.
Tunaamini wapo wanaopoteza maisha kwa sababu hawana fedha za matibabu na iwapo wangekuwa na bima ya afya wangeendelea kuishi, lakini familia zimejikuta kwenye mzigo wa madeni kwa ajili ya kutafuta fedha za kugharamia matibabu kwa ndugu yao.
Wengine wameuza mali na hali huwa mbaya zaidi pale mtu anapofariki kwa kuwa familia hutakiwa kulipa deni kwanza ndipo wakabidhiwe mwili wa ndugu yao, matukio ambayo yanaongezeka licha ya kila hospitali kueleza kuwa kuna utaratibu wa kufuata ili kupata msamaha.
Iwapo mtu huyu angekuwa na bima ya afya maana yake angekuwa ameshajikusanyia fedha zinazomwezesha kugharamia matibabu, lakini kwa wale ambao wanalipia bima, lakini hawaugui kwa miaka mingi maana yake zinasaidia kugharamia matibabu ya wengine.
Kuna umuhimu mkubwa kuwa na Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwa italeta manufaa makubwa kwa wengi kwa kuwa sasa nguvu kazi itakuwa na uhakika wa matibabu na kuwa na afya njema muda wote, maana yake watawajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao.
Tunaamini iwapo Muswada wa Sheria hii utawasilishwa bungeni, utakuwa umeshirikisha wadau wote muhimu kwa kutokana na umuhimu wa suala hilo na pia kutakuwa na ushiriki wa sekta binafsi.
Aidha, muswada huo ukifikishwa bungeni sasa utakuwa ni wajibu wa watunga sheria kuuangalia kwa jicho la uwakilishi wa wananchi wao, kwa kuhakikisha mambo yote ya msingi yamejumuishwa ili inapoanza kutekelezwa kama sheria rasmi kusiwe na changamoto au mkwamo.
Hivyo, tunaona kauli ya Spika ya kuitaka serikali kuharakisha mchakato huo ni muhimu sana, tukiamini kuwa moja ya vipaumbele vya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni afya za wananchi.
Tunaamini kuwa kila Mtanzania akiwa na bima itakuwa rahisi kwake kupata huduma za afya na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo yake na taifa kwa ujumla.
Ni imani yetu muswada huo ukifikishwa bungeni, wabunge watatekeleza wajibu wao kwa kuupitisha haraka, kwa kuwa wanaelewa vikwazo wanavyokumbana navyo wananchi wao katika kupata huduma za afya.










