Licha ya kuwapo juhudi mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko hayo, changamoto bado ni kubwa na inapotokea uhaba wa mvua unaombatana na upepo mkali kama ilivyokuwa mwaka huu wananchi wanaathirika.
Miongoni mwa juhudi ambazo zimechukuliwa na serikali ni kuibua vyanzo vipya vya maji katika kukabiliana na upungufu wa huduma hiyo unaotokana na jua, upepo na ukosefu wa mvua kuathiri sekta ya maji.
Mkoani Dar es Salaam, juhudi za kuongeza maji kupitia mradi wa visima virefu vya Mpera na Kimbiji kufanikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo mengine ya Temeke.
Kadhalika ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji la Kidunda mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha yanakuwapo maji ya kutosha wakati wote bila kujali ni masika au kiangazi kwa watu wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Lakini shida ya maji bado haijaisha. Tunaona kuwa kazi zaidi na ubunifu unahitajika. Vyanzo vya maji vya Ruvu na Wami ambavyo hulisha Dar es Salaam na Pwani vimepungua, lakini kwa Tanzania nzima mabadiliko hayo, ukataji miti na uharibifu wa mazingira na kilimo na ufugaji kwenye maeneo jirani na mito yameendelea kuwa tishio kwa usalama na upatikanaji wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA, imeshatoa mwelekeo wa hali ya mvua na kutaja uwepo wa vipindi virefu vya ukame kuanzia sasa hadi Januari mwakani yote haya yanatishia hatima ya maji nchini na kwa mazingira hayo ni wazi kuwa Mamlaka za Maji, Usafi wa Mazingira Mijini zina kazi kubwa kufikiria namna ya kumaliza changamoto ya maji mijini huku Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) nao ukitakiwa kubuni na kutekeleza mikakati ya kumaliza shida ya maji vijijini.
Kwa hali kama hiyo, tunaishauri serikali kuanza sasa kulifanyia kazi suala la kuhifadhi maji mengi ya mvua yanayopotea kila mwaka ili wananchi wasipate shida hasa nyakati za ukame.
Mvua zinazonyesha na hata kuwa juu ya viwango na mafuriko yanayotokea sehemu nyingine, yote hayo ni maji yanayopotea. Ndiyo maana tunaomba sasa serikali iamke na kuona namna bora ya kutunza mabilioni ya lita za maji ya mkvua yanayopotea kila mwaka kwa kuchimba mabwawa mengi zaidi na kuweka hifadhi za maji za taifa kwenye kanda, mikoa na wilaya.
Tunashauri zifanyike njia mbalimbali za uvunaji wa maji hayo ili yasipotee bure, bali yavunwe na kuhifadhiwa kwa ajili ya mahitaji ya baadaye badala ya kuacha yapotee kila mwaka huku wananchi wakikosa maji safi na salama.
Kwa mfano TMA inasema, kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.
Kutokana na mazingira kama hayo, ndiyo maana tunashauri kuongezwa kwa vyanzo vingi zaidi na kufanya juhudi za kuhifadhi maji, serikali iwekeze eneo hilo kwani uhaba huo unapelekea kuwepo magojwa na kuongeza gharama zaidi kwa serikali kwenye sekta ya afya.










