Pia Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, amesema kati ya watu wanaougua 10, vifo saba vinatokea kwa watu ambao hawajachanja na kuwataka Watanzania kuchanja ili kuwa salama kwa kuwa chanjo zipo na lengo la serikali ni kuwafikia watu zaidi ya milioni 35.
Taarifa hizi za wazi zilizotolewa na serikali za hali ya maambukizi nchini, zitaamsha wengi kuchukua hatua ya kujikinga na kwenda kuchanja.
Kwa ujumla hali sio nzuri kwa kuwa sasa serikali inadhihirisha kuwa janga hilo limerudi kwa kasi nchini, katika kipindi hiki ambacho Watanzania wengi wamekwenda vijijini na miji mingine kuungana na wanafamilia kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Itakumbukwa mwezi Machi, mwaka huu, mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara ilikuwa katika wakati mgumu kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya UVIKO-19, katika kipindi ambacho kulikuwa na baridi.
Wataalamu wanasema kirusi hicho hupata nguvu kwenye baridi na ndiyo maana kumekuwa na kupanda na kushuka kwa maambukizi kutegemeana na hali ya hewa.
Ni muhimu sana serikali na viongozi wa dini ikahimiza watu watakaoshiriki ibada za mwisho wa mwaka au Ijumaa na Jumapili, kuhakikisha wanaingia maeneo hayo wakiwa wamevaa barakoa, kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono.
Pia kwenye sherehe mbalimbali tahadhari ichukuliwe ipasavyo ili kuhakikisha waliokwenda vijijini hawawi sehemu ya chimbuko la kusambaza maambukizi kwenda vijijini au kwenda mjini.
Hali hii haikwepeki kuhimiza watu kuchanja hata kwa wataalamu kupata nafasi kwenye nyumba za ibada kueleza umuhimu wa chanjo na faida ya kuchanja ili kuongeza idadi ya wanaochanja.
Tunaamini ikiwa kasi ya kuelimisha umma kwa mifano halisi kutasaidia wengi kuelewa umuhimu na kuchukua hatua ya kuchanjwa kwa kuwa kila mmoja anataka kuendelea kuishi.
Lazima tuwaeleze watu mifano ya nchi za Afrika zilizofanikiwa kwenye chanjo, Ulaya na Marekani ambao sasa wanaishi bila hofu kwa kuwa wengi au wote wamepata chanjo.
Kama wao wameweza basi hata Tanzania inaweza kuingia kwenye historia ya kuchanja watu wengi na kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 na kila mtu kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Ni vyema watu wakatambua kuwa hata kama utachanja ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa hata ukichanja unaweza kupata maambukizi, lakini haitakuwa makali kama ambaye hajachanja.
Ipo mifano hai ya ambao hawajachanja walivyopata ugonjwa huo na ambao wamechanja, kwa ambao wamechanja wameugua lakini hawakulazwa au kuwekewa mashine ya kuwasaidia kupumua na kulazwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Ikiwa nyumba za ibada, sokoni, kwenye minada na kwingine kutatumika vyema kutoa elimu ya kujikinga na kuchanja, tunaamini Watanzania wengi watachanja na kuwa salama zaidi.
Lazima kutoa elimu sahihi ili kuondoa hisia mbaya zilizojaa kwenye vichwa vya watu kuwa chanjo sio salama na mengineyo ambayo yamerudisha nyuma utayari wa watu kuipokea na kukubali chanjo licha ya kwamba ni bure.










