Viongozi, wachezaji tumieni vyema dirisha dogo la usajili

25Dec 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi, wachezaji tumieni vyema dirisha dogo la usajili

WAKATI mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ukiwa unaendelea, tayari Shirikisho la Soka Nchini (TFF), limeshafungua dirisha dogo la usajili kwa klabu zinazotaka kuimarisha vikosi vyake.

Dirisha hilo lilifunguliwa tangu Desemba 15, mwaka huu na linatarajiwa kufungwa ifikapo Januari 15, mwakani.

Usajili huo wa dirisha dogo unahusisha pia na timu za Ligi ya Championship, First League pamoja na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, lakini tu kwa timu ambazo zilikuwa hazijatimiza idadi ya wachezaji wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni.

Lengo la usajili huo si kutoa nafasi ya kuimarisha vikosi vya timu hizo zinazoshiriki ligi mbalimbali za hapa nchini, ni kutaka kufikia malengo ya msimu husika kwa mwelekeo wa wanaowania ubingwa kuanza kuonekana au kwa wale wanaotakiwa kuanza kupambana kujiondoa mkiani.

Kila timu inatakiwa isajili wachezaji kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi ambalo lenyewe ndio linafahamu vyema mapungufu yaliyoko kwenye kikosi husika na si kiongozi wa klabu, mwanachama au shabiki.

Mchakato huu unahitaji kufanyiwa kazi kiweledi kwa sababu matokeo yake huonekana hadharani na majibu hupatikana mwishoni mwa msimu, klabu itakayokosea katika zoezi hili, ni wazi itajiweka kwenye wakati mgumu wa kufanya vyema.

Tunatarajia kuona klabu, wachezaji na makocha wanalitendea haki dirisha hili la usajili kwa kila mmoja kufanya majukumu yanayomhusu ili malengo yanayokusudiwa yafikiwe ipasavyo. Kuingilia majukumu ya mwingine, ni moja ya sababu ambayo inaweza kuizamisha timu.

Huku kukiwa na udhamini mnono wa Azam Media ambao umetangaza kutoa zawadi ya fedha mpaka kwa timu itakayonusurika na janga la kushuka daraja, tunatarajia kuona ushindani unaongezeka katika michezo inayoendelea na hatimaye timu itakayostahili kupata ubingwa ipate.

Mbali na klabu, wachezaji wanatakiwa kufanya maamuzi sahihi ya kujiunga na timu ambazo zitawapa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao na kuacha kuangalia upande mmoja tu wa maslahi.

Hii imewatokea wachezaji wengi wanaokubali kutoka timu A na kujiunga na timu B bila kuangalia hatima yake ya baadaye. Viongozi wa klabu ni kama wazazi, ni vyema mkawa makini katika kusajili wachezaji ambao watatumika na si kuchukua wachezaji ambao uhakika wa kupata namba ni mdogo.

Mbaya zaidi usajili huu unawagusa zaidi wachezaji chipukizi wa Kitanzania ambao taifa linawategemea kupeperusha bendera ya nchi katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Nipashe tunazikumbusha klabu zinazowasajili nyota chipukizi, lakini wanakosa namba kwenye timu hizo, kuwatoa kwa mkopo kwa klabu nyingine ili kuendeleza vipaji vyao badala ya kuwaacha wakikaa benchi kwa muda mrefu au kuacha kuwasajili kwa 'mihemko'.

Tunaamini soka la sasa ni la ushindani, na ili mchezaji aonyeshe kiwango bora au akabiliane na ushindani kutoka kwa timu pinzani ni lazima apate nafasi ya kucheza mara kwa mara, kumsajili mchezaji bila ya kumhakikishia nafasi ya kucheza ni kutomtendea haki maana kipaji chake kitakuwa kimejiweka njia panda.

Si lazima kila mchezaji asajiliwe timu kubwa au kongwe, mchezaji anayejituma anaweza kuonekana na mawakala na makocha wa nje ya nchi endapo atapata nafasi ya kucheza kwa sababu michezo yote ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inaonekana kwenye televisheni.

Mchezaji kama Ditram Nchimbi akiwa Polisi Tanzania alikuwa ni tegemeo, lakini aliposajiliwa Yanga, kwake nafasi ya kucheza ilikuwa adimu na hivyo kupoteza namba hadi kwenye kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), lakini baada ya 'kuzinduka' na kukubali kuondoka klabuni hapo kupitia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa, amekuwa ni mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Geita Gold FC ambacho kilikuwa na hali mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Huu ni wakati wa kila mmoja kutafakari kabla ya kukubali kusaini mkataba wa kujiunga na timu yoyote katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.