Pia, kuwalinda wazee na watu wengine wenye maradhi yasiyoambukiza ambao ni kundi lililo hatarini zaidi kwa kipindi hiki ambacho kuna mikusanyiko ya watu.
Kadhalika, wazazi wametakiwa kuwalinda watoto walio kwenye kipindi hiki cha likizo ambao watasafiri kwenda maeneo mengine nchini, kwa kuhakikisha wanavaa barakoa, kunawa mikono na kuepuka misongamano.
Tangu kugundulika kwa ugonjwa wa UVIKO-19 matangazo ya kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ni mengi, na yamezidi zaidi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuwa Tanzania kuna ugonjwa huo, akaonyesha mfano kwa kuchanja na kuvaa barakoa kila anapokuwa kwenye mikusanyiko.
Kwenye vituo vya mabasi kuna vyombo vya kunawa mikono ambavyo havitumiki, licha ya hamasa ya kuchukua tahadhari watu hawavai barakoa wala kutakasa mikono wanapokuwa kwenye mikusanyiko.
Tunashauri serikali kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo lake ili kuepusha janga kwa wazee na makundi mengine yaliyo kwenye hatari huko vijijini, kwa kuwa wengi bila kujua hawatakumbuka kunawa au kuvaa barakoa.
Utekelezaji ni pamoja na kukagua mabasi mara kwa mara kama watu wanavaa barakoa na ikiwezekana kuchukua hatua kwa makondakta na madereva ambao hawahimizi uvaaji barakoa.
Mabasi mengi kwa sasa yana viyoyozi (AC) na watu wanakaa kwa zaidi ya saa tatu safarini, ni kawaida kukuta basi zima hawajavaa barakoa na wanashuka vituo mbalimbali, jambo ambalo ni hatari kwa kuwa wataalamu wanatueleza kuwa kirusi hicho huimarika zaidi kwenye baridi.
Ili kufanikisha utekelezaji ni lazima kuwe na ufuatilia wa karibu wa mabasi kutoa matangazo ya mara kwa mara kwa abiria kuvaa barakoa, lakini Polisi wa Usalama Barabarani pamoja na mambo mengine wanayokagua ni vyema wakahimiza uvaaji barakoa au mabasi kufungua vioo ili hewa ya asili iingie.
Mathalani, Nipashe ilitembelea Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli na vingine nchini na kubaini kuwapo kwa vyombo vya kunawa mikono, lakini havitumiki, msongamano mkubwa wa watu na wengi hawavai barakoa jambo linalosababisha maambukizi kusambaa.
Nguvu inayotumika kuhimiza watu kuvaa barakoa wanapokuwa ndani ya viwanja vya ndege, boti na wanapoingia kwenye ofisi za serikali, sasa ielekezwe kwenye vyombo vya usafiri wa barabara na masoko ili kuepusha kusambaa kwa kirusi hicho, hasa katika kipindi hiki tunachoelezwa kuwa kuna kirusi kipya cha Omicron.
Kwa kuvaa barakoa, kuchanja na kunawa mikono mara kwa mara kumesaidia baadhi ya nchi zilizo mstari wa mbele kwenye kukinga raia wake dhidi ya UVIKO-19 kama Uingereza kuruhusu mashabiki wa mpira kuingia uwanjani bila barakoa kwa kuwa wamefanikiwa kuchanja watu wote.
Hii ni uthibitisho kuwa ikiwa tahadhari itachukuliwa inavyotakiwa basi tutafanikiwa kupambana na UVIKO 19 hasa kipindi hiki watu wanaposafiri kwenda kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka.
Hadi Desemba 18, mwaka huu, jumla ya wananchi 1,275,795 sawa na asilimia 2.21 walikuwa wamepata chanjo ya Uviko-19, huku lengo likiwa ni kufikia watu milioni 35 sawa na asilimia 60.










