Ligi hiyo ilikuwa na changamoto nyingi hasazile zilizokuwa zikisababishwa na Shirikisho la soka nchini (TFF) husuani suala la upangaji ratiba ambapo tumeshuhudia ratiba ya ligi hiyo ikibadilishwa kila wakati kwa sababu mbalimbali ikiwemo uwepo wa mashindano ya kimataifa.
Nipashe tunaamini kwa kiasi kikubwa mapungufu hayo yalichangia kupunguza msisimko wa ligi yenyewe.
Ni vyema basi TFF ikijipanga mapema na kuhakikisha wanaingiza kwenye kalenda yao matukio mbalimbali ikwemo mashindano ya kimataifa ambayo klabu au timu ya taifa itashiriki ili kuondoa tatizo la kubadili kila wakati ratiba ya ligi kuu.
Mashindano kama klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), Chalenji na ushiriki wa klabu zetu kwenye michuano Shirikisho la soka Afrika (CAF) yatazamwe wakati wa kuandaa ratiba ya ligi kuu kwa msimu ujao.
Tuige mfano kwa nchi za wenzetu ambao upangaji wa ratiba za ligi zao unatokana na mashindano ya kimataifa kukwepa kupangua pangua ratiba kama inavyotokea hapa nyumbani.
Nipashe tunaamini mambo kama haya ambayo yanaepukika yanaweza yakafanywa na TFF na kujikuta ligi yetu ikiendelea bila kuona sarakasi kwenye ratiba yetu.
Msimu huu uliomalizika hivi karibuni tumeshuhudia viporo vikiwa vingi na kujikuta timu moja na inakuwa na viporo mpaka vinne kitu ambacho si sahihi.
Viporo hivyo vilitokana na ushiriki wa klabu za Azam na Yanga kwenye mashindano ya kimataifa ambayo yalikuwa yanajulikana mapema.
Tunaomba TFF kuwa makini katika jambo hili ili kuongeza msisimko kwenye ligi yetu, ni vizuri maandalizi yake yakafanywa sasa hivi kwa kuangalia ratiba ya michuano ya kimataifa.
Lakini mbali na changamoto hizo, TFF imejitahidi kuendesha ligi vizuri kupitia kwa bodi ya ligi kuu na Nipashe tunaamini bado vyombo hivyo vinauwezo wa kufanya vizuri zaidi ya hapa kwa msimu ujao.
Ni wazi kuwa ligi bora inajengwa na Shirikisho la soka, timu husika na wadau wa soka, tunategemea ligi bora msimu ujao na kumalizika kwa ligi msimu huu kuwe mwanzo wa maandalizi ya ligi ya msimu ujao.
Vile vile kwa sasa ni wakati wa klabu zetu zitakazoshiriki ligi kuu msimu ujao kuanza maandalizi yake sasa hivi ikiwa ni pamoja na kufanya usajili mzuri na wenye tija pamoja na kuweka mikakati kwa ajili ya msimu ujao.
Klabu zifanye usajili kwa kufuata maoni na matakwa ya makocha wao na kuacha kasumba ya viongozi kuingilia usajili wa timu zao.










