Hatua zichukuliwe kudhibiti mauaji ya kuchinja nchini

31May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua zichukuliwe kudhibiti mauaji ya kuchinja nchini

KATIKA toleo letu la jana tulichapisha habari kuhusiana na kasi ya matukio ya mauaji ya watu kwa kukatwakatwa kwa mapanga na kuchinjwa katika maeneo kadhaa nchini.

Katika kipindi cha mwezi Mei mwaka huu, kulikuwa na matukio matano ya watu kuuawa kwa kuchinjwa au kukatwakatwa kwa mapanga, chanzo kikidaiwa kuwa ni kulipiza visasi.

Tukio la hivi karibuni kabisa ni la mtumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Anethe Msuya (30), aliyeuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana, Kigamboni, Dar es Salaam, Mei 26.

Mei 25, Saidi Simba (mume) na Kadogo Ehicho (mke) waliuawa kikatili katika Kijiji cha Mmazami, Butiama mkoani Mara kwa kukatwa na mapanga wakiwa wamelala.

Mei 19, watu 15 kundi la wahalifu wakiwa wameficha nyuso zao, walivamia msikiti katika mtaa wa Utemini wilayani Nyamagana, Mwanza na kuwaua watu watatu waliokuwa wakifanya ibada usiku kwa kuwakata kwa mapanga na shoka.

Mei 11, watu saba wa familia moja waliuawa wilayani Sengerema, Mwanza kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Kadhalika, Mei 5, watoto wanne wa familia moja katika kijiji cha Msufini, wilayani Same, Kilimanjaro, waliuawa kwa kukatwakatwa wakiwa wamelala, baada ya kuvamiwa na mtu anayedaiwa kuwa ni ndugu yao.

Katika mtiririko huu wa mauaji haya ya kikatili yanayotokea kwa kasi, ni wazi kwamba kuna sababu kubwa zinazochangia, achilia mbali madai ya kulipiza visasi.

Tunapata shaka kuamini moja kwa moja kuwa mauaji hayo ya kikatili na ya kinyama sababu kubwa ni kutokana na kulipiza visasi kwani haiwezekani ulipizaji wa kisasi uwe ni kumchinja binadamu au kukmatakata kwa mapanga au shoka.

Tunachoamini ni kwamba sababu kubwa inayochangia ukatili huu ni mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao unaikabili jamii yetu, kiasi kwamba watu kadhaa wameacha kumuogopa Mungu, hivyo kama taifa hatunabudi kujitafakari upya na kuchukua hatua za kurejea katika maadili.

Kuna matukio mengine ya kikatili ambayo yamekuwa yanatokea nchini, yakiwamo mauaji ya vikongwe, watu wenye ulemavu wa ngozi na kuchukuliwa kuwa sababu ni imani za kishirikina, hilo halina mjadala kwa kuwa watu wachache kwa imani potofu wanaamini watapata utajiri na uongozi.

Kuna baadhi ya waliotoa maoni kuhusiana na sababu za mauaji ya kukatakata watu mapanga pamoja na kuwachinja na kusema sababu ni visasi vinavyotokana na kudhulumiana mali ndani ya familia, mapenzi na uonevu.

Mmoja wa viongozi wa dini alisema jambo la msingi ni upotofu maadili unaotokana na malezi hasi ya watoto umesababisha ukatili kuendelea hadi ndani ya familia na vyombo vinavyohusika kutochukua hatua kwa wakati mwafaka, kwa kuwa wasipokemea wala sheria kuwabana, wataendelea kusababisha mauaji.

Binadamu pamoja na kuwa ameumbwa kama wanyama, lakini anatofautiana na wamyama kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ana utashi wa kujitambua na kujua mambo gani ni mazuri na yapi ni mabaya, hivyo hapaswi kuwa na roho ya ukatili.

Kutokana na hali hiyo, tunaona kuna haja kwa jamii nzima kuchukua hatua madhubuti ili kudhibiti matukio haya ya ukatili wa kinyama.

Miongoni mwa hatua hizo ni kwa viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao ubaya ya kuua binadamu wenzao na kuwakumbusha kufuata maadili, maofisa wa serikali hususan wa ustawi wa jamii popote walipo kushirikiana na asasi za kiraia kutoa elimu kuhusu haki za binadamu na familia zihakikishe zinahimiza malezi bora kwa watoto ili wasijifunze tabia ya ukatili.

Vyombo vya dola navyo tunavishauri kuimarisha intelijensia kubaini viashiria vya kutokea matukio hayo na kuyadhibiti mapema.