Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Injinia Felchesmi Mramba, kiwango cha wizi wa umeme kimepungua kutoka asilimia 23 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 17.
Jitihada kadhaa zilizofanywa katika kipindi hicho ndizo zilizopunguza wizi huo ambao huigharimu Tanesco mabilioni ya fedha, mbali na athari mbalimbali ambazo huwakuta pia watumiaji halali wa nishati hiyo.
Hakika, taarifa hiyo inaashiria mafanikio makubwa. Sisi tunapongeza jitihada hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimetokana na kuongezeka kwa matumizi ya teknolijia ya mita za Luku ambazo hufungwa kwa juu, nje ya nyumba za watumiaji.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, sisi tunaamini kuwa bado kuna kila sababu ya kuongeza nguvu katika kukomesha wizi wa umeme.
Kwamba, mbali na jitihada za Tanesco, ushiriki wa wananachi wa kawaida na hasa watumiaji wa umeme, unapaswa kuwa wa juu. Lengo kuu liwe ni kumaliza kabisa wizi wa umeme ili wizi huo upungue hadi kufikia asilimia sifuri.
Hata hivyo, kwa kutambua kuwa ni vigumu kutimiza lengo kwa ukamilifu wa asilimia 100, sisi tunaona kuwa hivi sasa ipo haja ya kuona walau kuwe na lengo mahsusi la kupunguza wizi wa nishati hiyo hadi kufikia kiwango cha chini ya asilimia 10.
Hilo linawezekana, muhimu ni kuhakikisha kuwa jitihada kadhaa zilizokwishaanza kitambo katika kudhibiti wizi wa umeme zinaungwa mkono.
Sisi tunasisitiza hili kutokana na ukweli kuwa athari zitokanazo na wizi wa umeme ni kubwa na kamwe hazibebwi na Tanesco peke yake. Bali, waathirika wa wizi wa umeme huwa ni pamoja na kundi kubwa la Watanzania wasiokuwa na hatia.
Kwa mfano, kuna kilio cha tatizo la kuwapo kwa umeme mdogo katika baadhi ya maeneo. Kwa mujibu wa wataalamu wa umeme, tatizo hili hutokana na sababu nyingi, na mojawapo ni kuwapo kwa watumiaji wa umeme wa wizi ambao mara zote, majina yao huwa hayamo katika orodha rasmi ya Tanesco.
Kwa kawaida, kiwango cha umeme hufikishwa mahala kulingana na mahitaji. Maana yake, kama takwimu za Tanesco zinaonyesha kuwa wateja wa umeme katika eneo fulani ni 5,000, kwa mfano; halafu ikatokea kuwa idadi hiyo siyo halisi kwa sababu kuna watumiaji wengine zaidi ya 3,000 hutumia umeme huo kwa njia za wizi, ni dhahiri kuwa makadirio ya Tanesco yanaweza kuwa potofu kwa sababu transfoma itakayofungwa yaweza kuwafikishia umeme wa kukidhi mahitaji ya watumiaji 5,000 tu na siyo zaidi ya hao waliomo kwenye kumbukumbu zao.
Matokeo yake, mbali na athari watakazozipata Tanesco kibiashara, wananachi wa kawaida ambao ni watumiaji halali wataathirika pia kwa sababu watapata umeme mdogo usiolingana na mahitaji, chanzo kikiwa ni ongezeko la idadi ya watumiaji wa umeme wa wizi.
Ni dhahiri kuwa wananchi wa eneo la namna hiyo hawatakuwa na uhakika wa kuhifadhi vyakula kwa usalama wkenye majokovu yao ya umeme.
Vinyozi wanaolipia umeme kihalali watashindwa kufanya shughuli zao na kujiingizia kipato, sawa na athari watakazozipata watumiaji wengine halali kama waendeshao biashara za migahawa ya chakula.
Hata nyakati usiku, hali ya usalama huwa shakani pia kwa sababu mwanga wa taa huwa na nuru hafifu mithili ya vibatari.
Kwa ufupi, wakazi wa eneo linalopata umeme mdogo kwa sababu ya wizi wa umeme hukumbwa na athari kubwa za kiuchumi na kijamii.
Ni katika mazingira kama hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa kuna kila sababu ya kuunga mkono vita dhidi ya wezi wa umeme kwa kuwafichua ili wachukuliwe hatua zinazostahili..










