Sputanza isimamieni hili kwa umakini mkubwa sana

27Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sputanza isimamieni hili kwa umakini mkubwa sana

CHAMA cha Wachezaji Soka Tanzania (Sputanza), kimepinga hatua za baadhi ya klabu zinazotaka kuwatoa wachezaji wake kwa mkopo bila wao kukubali.

Mwenyekiti wa chama hicho, Mussa Kisoki, amenukuliwa akisema, ili klabu imtoe mchezaji kwa mkopo kwenda kwenye klabu nyingine ni lazima mwenyewe aridhie na kitendo cha kumlazimisha ni kosa, ambapo sisi pia tunaunga mkono.

Kauli ya Kisoki, imekuja baada ya kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa klabu mbalimbali zinatarajia kuwatoa wachezaji wao kwa mkopo kwenda kwenye klabu zingine ikiwa ni siku chache tu kabla ya dirisha kubwa la usajili kufungwa.

Kwa mujibu wa Kisoki, mchezaji ana haki ya kuhoji anakopelekwa, kule anakokwenda ni lazima ajue anaenda kuongeza kipaji chake au kuua, au anakwenda kuongeza kipato chake, au kitapungua.

Na kwamba, asiporidhia ni lazima abaki na timu yake, au uvunje mkataba kwa kumlipa mshahara wake wote wa muda waliomsajili na fedha yake ya usajili.

Katika hili, Nipashe tunaiunga mkono Sputanza kwa asilimia 100, kwa sababu mtindo huu ukiendelea kuchekewa athari zake ni kubwa sana kwa wachezaji wetu kwa siku za usoni.

Timu kubwa hasa Simba na Yanga zimekuwa na tabia ya kumtaka kila mchezaji wanayemwona mbele yao, matokeo yake hujikuta wamefanya usajili wa wachezaji ambao hawakuwa wakiwahitaji au kujaza wachezaji wengi kwenye nafasi moja.

Kwa maneno mengine timu hizi kubwa zinapenda kufanya usajili wa kukomoana kwa kuwahi kila mchezaji ambaye anaonekana kuwa na kiwango cha juu, hata kama hawana mahitaji nae.

Matokeo yake mfumo wa kocha unakuwa tofauti na wachezaji aliowakuta na hivyo kulazimika wengine kuwakataa na pale timu inaposhindwa pakuwapeleka, hulazimika kuingia makubaliano ya kuwatoa kwa mkopo.

Tofauti ya mikopo iliyozoeleka kwa ligi zilizoendelea na hii yetu ni kwamba, kwanza mchezaji analazimishwa kuondoka, pili analazimishwa kukubali kupunguziwa mshahara wake kama atataka kubakia na timu husika.

Kiukweli hiyo siyo haki hata kidogo, kwa sababu kila mchezaji ndoto zake ni kukuza kipaji chake ili afikie kiwango cha juu kabisa na ikiwezekana hata kupata timu nje ya nchi.

Ikumbukwe kwamba, soka ndio ajira yake na ina ukomo wa umri, mchezaji hupendelea kwenda kujiunga na timu kubwa ili aweze kuongeza kipato chake kwa upande wa mshahara na marupurupu mengine.

Hivyo, suala la kumlazimisha mchezaji kuondoka au kupunguziwa mshahara wake maana yake unamnyima haki yake kimsingi na kumrudisha nyuma kabisa katika ndoto zake alizojiwekea.

Taarifa za hivi karibuni zinaonesha kuwa kunaweza kukawa na kesi nyingi baada ya dirisha la usajili kufungwa Agosti 31, mwaka huu.

Kwani, taarifa zinasema kuna wachezaji wengi wamegoma kuondoka kwenye klabu walizosajiliwa, kwa sababu kule wanakotaka kupelekwa hawaoni kama kunaweza kuwaimarisha kisoka.

Nipashe, tukiwa kama wadau wakuu wa mchezo wa soka, tunazishauri klabu kukaa na kuzungumza na kufikia makubaliano na mchezaji husika kama wanataka kumtoa kwa mkopo.

Lakini, kubwa ni kwamba, lazima maslahi yake yaangaliwe kwa umakini mkubwa, kwa sababu kumtoa kwa timu moja kwenda nyingine bila idhini yake ni sawa na kummaliza au kumuua kabisa kisoka.

Hivyo wito uliotolewa na Sputanza unatakiwa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa ili kuweza kuboresha soka letu kufikia viwango vya kimataifa ambavyo kama nchi tumekuwa tukiviota kwa muda mrefu.

Pia, wachezaji wenyewe wanatakiwa kuwa makini na mikataba ambayo wanaingia na timu hizo na pia kutokukubali kirahisi kuhamishwa timu au kukatwa mishahara yao.

Kubwa wanaloweza kufanya ni kufikia makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba walioingia ili waweze kulipwa stahiki zao zote na kuendelea kutafuta maisha na kukuza vipaji vyao vya uchezaji katika timu nyingine.

Nalo shirikisho la soka Tanzania, TFF, ambalo ndio mlezi na msimamizi mkuu wa timu zote, linatakiwa  kuwa mstari wa mbele katika kulisemea hilo, ili kama mchezaji na klabu wanataka kuachana, basi waachane kwa utaribu ulionyooka na wenye maslahi kwa pande zote mbili.