Simba Queens imekata tiketi hiyo baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya kuwania kushiriki fainali hizo za Afrika kwa Wanawake kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), iliyomalizika Jumamosi iliyopita hapa nchini.
Kwa mantiki hiyo, Simba Queens sasa itakuwa timu pekee itakayouwakilisha Ukanda wa CECAFA kwenye michuano hiyo ya Afrika ambayo itafanyika nchini Morocco Oktoba mwaka huu ikishirikisha jumla ya timu nane.
Timu sita kati hizo nane, zinapatikana kutoka kanda tofauti za Afrika ambapo kwa CECAFA rasmi sasa ni Simba Queens, Ukanda wa COSAFA ni Green Buffaloes ya Zambia, Ukanda wa UNAF ni Wadi Degla ya Misri, wakati Ukanda wa WAFU A ni Determine Girls ya Liberia.
Bado kanda mbili hazijapata wawakilishi rasmi, ambazo ni Ukanda wa WAFU B ambapo bingwa atapatikana Septemba 2, nchini Ivory Coast huku Ukanda wa UNIFFAC bingwa akitarajiwa kupatikana Septemba 4, mwaka huu nchini Cameroon.
Ikumbukwe pia kuna timu nyingine mbili zilizoingia moja kwa moja ili kufanya idadi kuwa nane, ambazo ni bingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini Morocco, AS FAR Rabat, iliyoingia kama timu mwenyeji pamoja na Mamelod Sundown ya Afrika Kusini, ambayo ni washindi wa pili wa COSAFA walioingia kama bingwa mtetezi.
Kwa orodha hiyo tu ya awali kabla ya kupatikana timu mbili shiriki katika fainali hizo za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Upande wa Wanawake, inaonyesha si michuano rahisi hata kidogo na yanahitajika maandalizi makubwa kwa wawakilishi wa Tanzania, Simba Queens.
Hata hivyo, kwa ubora ulionyeshwa na Simba Queens kwenye kinyang'anyiro cha upande wa CECAFA kuwania kufuzu fainali hizo, tunaamini kama maandalizi yataanzia hapo ilipoishia na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo, haitatuangusha katika michuano ya CAF.
Matarajio hayo makubwa kwetu yanatokana hasa na ubora ulioonyeshwa na wachezaji wa Simba Queens kwa kushinda mechi zote tano kuanzia hatua ya makundi hadi fainali ilipotwaa ubingwa huo wa CECAFA Jumamosi iliyopita.
Lakini si hilo tu, bali pia kama timu ilionyesha ubora zaidi kuanzia safu ya ulinzi hadi ya ushambuliaji, kwani iliruhusu bao moja tu huku ikifunga jumla la mabao 18, hivyo Simba Queens si ya kubeza hata kidogo, ingawa inatakiwa pia itambue sasa inakwenda kukutana na mabingwa kutoka kila kanda.
Kutokana na hilo, ndilo linalotufanya kuwakumbusha kuanzia wachezaji, benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na uongozi mzima wa klabu ya Simba, kuhakikisha yanafanyika maandalizi makubwa zaidi kuelekea michuano hiyo kwani tunachotaka kukishuhudia nchini Morocco ni kuona timu hiyo ikifika fainali na kutwaa taji hilo.
Tunaamini hilo linawezekana kama kila mmoja katika timu hiyo atabeba majukumu yake ipasavyo kuanzia nje ya uwanja na ndani ya uwanja hususan kuitafutia mechi nyingi na kubwa zaidi za kirafiki ili kuwaweka wachezaji fiti kuelekea fainali hizo.
Ni wazi michuano ya CECAFA iliyomalizika, imeonyesha ni wapi ambapo panavuja kuelekea fainali hizo za Afrika, hivyo katika kipindi hiki cha mwezi mmoja wa ushee, tunaamini benchi la ufundi linaweza kutafuta suluhisho kwa kuangalia namna ya kupaziba ili kukiimarisha kikosi chao.
Lengo letu ni kuona Simba Queens inatangaza vema soka letu kupitia michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika kwa ngazi ya klabu kwa upande wa wanawake, lakini ni wakati wa wachezaji kila mmoja kwa wakati wake kujituma na kutozembea mazoezini, kwani kupitia fainali hizo za CAF, ni sehemu sahihi kwao kujitangaza na kupata klabu kubwa nje na ndani ya Afrika kwa maslahi yao binafsi na taifa pia.









