Madai ya kukosa nyumba wananchi Magomeni Kota yashughulikiwe kwa amani

26Aug 2022
Mhariri
Nipashe
Madai ya kukosa nyumba wananchi Magomeni Kota yashughulikiwe kwa amani

KATIKA gazeti la Nipashe toleo la jana, kulikuwa na habari kwamba wananchi  21 wanaodai kuwa wakazi halali wa nyumba za Magomeni Kota mkoani Dar es Salaam, wameulalamikia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuwa imewanyima nyumba wakati wana mikataba halali ya ukazi.

Licha ya kudai kukosa haki hiyo kama wenzao waliokuwa wameondolewa kupisha ujenzi wa nyumba mpya na kuleta mwonekano mzuri eneo hilo, wananchi hao wamedai kuwa TBA imewataka kama hawajaridhika waende mahakamani.

Kwa mujibu wa wananchi hao, baada ya kubaini kuwapo kwa tatizo hilo, walifuata hatua kuwasilisha kilio chao ikiwamo kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na TBA. Awali, walibainisha kuwa wapangaji waliokuwa na malalamiko ya kutorejeshwa katika nyumba hizo  walikuwa 44 lakini baada ya mchakato wa utatuzi walibaki 21 ambao ndio wameambiwa waende mahakamani kama wanaona hawajaridhika.

Pamoja na kauli hiyo ya TBA, taarifa ambayo wanadai waliipata kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni iliwahakikishia kuwa mgogoro umemalizika na kwamba watakabidhiwa nyaraka lakini wakashangaa kuona kuwa baadhi ya watu waliopewa hawakuwa wapangaji katika nyumba za awali ambazo zilibomolewa.

Jambo hilo limechukua mlolongo mrefu tangu wakati wa ubomoaji wa nyumba za kota zilizokuwa katika mwonekano wa kizamani kwani wapangaji hao waliwahi kuwa katika mvutano na serikali na hatimaye kuahidiwa kwamba watarejeshwa baada ya kujengwa nyumba za ghorofa ambazo zimebadilisha mandhari ya eneo hilo.

Ni muhimu jambo hilo likapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuleta amani na maelewano na wananchi hao ambao wengi waliishi miaka nenda rudi, wapatiwe haki kama ilivyokuwa kwa wenzao ambao wamepewa nyaraka na kuwa wapangaji, wakiendelea kufurahia ukaribu wao uliodumu kwa miaka mingi.

Pamoja na TBA kutoa kauli kwamba wanaolalamika si wapangaji, jambo la kujiuliza ni kwa nini waliwapa nyaraka za kurejea kwenye nyumba hizo ilhali hawakuwa wapangaji? Hapo kuna jambo ambalo limejificha linahitaji uwajibikaji kwa waliotoa kauli hiyo.

Ni imani yetu kwamba lengo la serikali katika kubadili mandhari ya eneo hilo ilikuwa njema kwani nyumba za awali, zilizokuwa zimepewa jina la ‘mabehewa’, zilikuwa na mwonekano wa kizamani na nyingi zilikuwa zimechakaa. Kwa mantiki hiyo, kujengwa upya kumeongeza thamani ya eneo pamoja na hadhi ya wananchi wanaoishi hapo, hivyo haki itendeke.

Kama alivyosema mwanasheria wa wananchi hao kuwa hawafikirii kwenda mahakamani bali watatumia njia za mazungumzo, ni vyema pande husika zikakutana na kujadiliana na hatimaye kumaliza suala hilo ambalo linaanza kutia doa mpango wa serikali.

Ni dhahiri kwamba kuna harufu ya ujanja unjana katika mgawo wa nyumba hizo, hivyo mamlaka za serikali zinapaswa kutolinyamazia suala hilo. Mamlaka zilizopewa dhamana ya kuisimamia haki na kuchunguza vitendo vyovyote vilivyo kinyume cha haki, ziingilie kati ili kupata ukweli wa suala zima na kama kuna watu wanatumia nafasi zao kwa manufaa binafsi, wachukuliwe hatua.

Katika serikali, kuna mifumo mbalimbali ya kiuongozi hivyo kuanzia ngazi ya wilaya, kwa maana ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni hadi serikali kuu kwa maana ya wizara zenye dhamana ya ardhi na majengo, ziingilie kati na hatimaye kumaliza mgogoro huo.