Matajiri wanaochochea mwendo kasi kwa madereva waadhibiwe

25Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Matajiri wanaochochea mwendo kasi kwa madereva waadhibiwe

KATIKA toleo letu la jana, tulichapisha habari iliyoeleza baadhi ya matajiri wa mabasi ya abiria wanavyochochea madereva wao kwenda mwendokasi ili wawahi kufika na kuwapa motisha ya bonasi.

Mabasi hayo ni yale yanayofanya safari zake kati ya Mwanza, Singida, Dodoma na Dar es Salaam na madereva wake wanashindana kwenda mwendokasi ili kuwahi kufika mapema kwa kuchochewa na bonasi inayodaiwa kutolewa na matajiri wa magari hayo.

Taarifa hiyo, ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Singida, wakati wa mazishi ya Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya Kinampanda, wilayani Iramba Winjuka Mkumbo, aliyepoteza maisha katika ajali iliyoua watu sita, wiki iliyopita.

Hali hii inasikitisha na hata wanaochochea na kusababisha ajali hizo wamekosa roho za kibinadamu kwa sababu wanaosafiri kwenye magari yao sio wanyama.

Kama ajali hizo zikiendelea kutokea na kumaliza uhai wa watu, hao abiria watatoka wapi wa kupanda mabasi yao.

Matukio ya mfululizo wa ajali yamekuwa yakiripotiwa kutoka katika mikoa mbalimbali, huku chanzo kikielezwa kuwa ni mwendokasi na baadhi ya madereva kutozingatia alama za barabarani.

Mashuhuda wa ajali hiyo iliyotokea Singida walizungumzia jinsi mabasi yanavyokuwa yakishindana kwenda mwendokasi kuwahi bonasi inayotolewa na matajiri wa mabasi hayo.

Wameiomba serikali kuliangalia jambo hilo na kulikomesha kwa kuwa baadhi ya matajiri wanawapatia fedha madereva wao kwa kuwashindanisha atakayewahi kufika wa kwanza kituoni.

Matajiri hawa wamekosa utu na wanachokiangalia ni faida pekee ili waweze kuongeza mabasi mengine na kuendelea kumaliza uhai wa watu wasiokuwa na hatia.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo iliyotokea Singida, amesimulia jinsi alivyojaribu kumwokoa diwani ambaye alikuwa bado hai na kumweleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni mwendokasi wa dereva.

Hata abiria walipojaribu kumwonya dereva huyo kupunguza mwendo, hakuwasikiliza na walipomkataa na basi hilo kuendeshwa na dereva mwingine wa akiba naye aliendesha mwendokasi zaidi ya dereva wa kwanza.

Inadaiwa tangu basi hilo likiondoka kituoni lilikuwa likiendeshwa kwa mwendokasi na kusababisha abiria kuwa roho juu.

Ujeuri au ubishi wa madereva hao, umeangamiza maisha ya watu waliokuwa wakitegemewa na familia zao na kuwaacha yatima.

Jeuri hiyo inasababishwa na matajiri hao wanaotoa bonasi ya fedha kuwachochea madereva wao waweze kwenda safari zaidi ya moja kwa siku, jambo ambalo linasababisha nguvukazi zinazotegemewa na taifa kupotezwa.

Ajali hizo zimesababisha viongozi mbalimbali wakiwamo wa madhehebu ya dini kukemea na kuwataka wahusika hasa kikosi cha usalama barabarani kuhakikisha ukaguzi wa mara kwa mara unafanyika kudhibiti ajali hizo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi alisema, halmashauri hiyo tangu itokee ajali hiyo na kumpoteza diwani wao imetoa ushirikiano na kugharamia mambo mbalimbali na kuomba madereva wawe makini wanapokuwa barabarani kwa kuwa wamebeba uhai wa watu wanaotegemewa na familia pamoja na taifa kwa ujumla.