Kilio cha watoto wanaoishi mazingira hatarishi kisikilizwe

24Aug 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kilio cha watoto wanaoishi mazingira hatarishi kisikilizwe

WATOTO wanaoishi mazingira hatarishi juzi walitoa kilio kwa makarani wa sensa walioanza kufanya zoezi la kuwahesabu usiku wa kuamkia jana, wakiiomba serikali kuwaunganisha na fursa za kiuchumi ikiwamo vyuo vya ufundi ili waondokane na mazingira ya kuishi na kufanya kazi hatarishi mtaani.

Kilio hicho cha watoto kinaonesha umuhimu wa sensa ya watu na makazi kufanyika ili kupata takwimu sahihi za watu wa rika zote kwa maendeleo yao.

Watoto hao zaidi ya 30 waliohesabiwa Manispaa ya Iringa, ni kielelezo cha wenzao wanaoishi katika mikoa tofauti kwenye mazingira hayo hatarishi.

Kilio chao kikubwa ni kuwa licha ya kuwa na vipaji, lakini bado wameishia kuwa ombaomba na kuishi mtaani kutokana na kukosa msaada.

Hamasa iliyokuwa ikitolewa ya kuwataka wananchi wote kushiriki sensa ya watu na makazi, bila kujali wanaishi katika mazingira gani, imewahamasisha watoto hao kujitoa kushiriki kuhesabiwa baada ya kujua umuhimu wake.

Wameamua kushiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi ili serikali izitambue kero wanazokumbana, ikiwa ni pamoja na kukosa makazi na kujikuta wakiishi na kufanyakazi mtaani.

Matumaini yao ni kuona serikali inawasaidia kutatua kero zao kwasababu wamesema wana vipaji vya kuimba, maigizo pamoja na ufundi, lakini wanakosa mtu wa kuwasaidia na kuishia kuokota makopo jalalani na kuyauza ili kujipatia chakula kitu ambacho ni hatari kwao.

Wanatamani kupata fursa ya kusoma na kuendelezwa ili waondokane na maisha hayo ambayo wakati mwingine huwaletea misukosuko ya kupigwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili.

Katika kilio chao wanasema wanakutana na majanga mbalimbali, lakini wanakosa msaada kutoka mamlaka kama serikali za mitaa na kata kutokana na kutotambuliwa kama wanavyotambuliwa watoto wengine.

Watoto wanaoishi katika mazingira hayo, baadhi yao hawakupenda kuishi hivyo, lakini kutokana na shida mbalimbali zinazotokea hujikuta wakiingia katika mazingira hayo.

Mara nyingi watu huwaona kama wahalifu kutokana na mwonekano wao na makundi wanayoambatana nao na wakati mwingine wakijikuta wakiangukia mikononi mwa polisi kwa kukosa mtetezi.

Kupitia sensa matarajio yao ni serikali kuwaunganisha na vituo mbalimbali vya kulea watoto pamoja na kuwapatia fursa ya elimu ili wasiwe tegemezi au kujihusisha na uhalifu.

Kupitia sensa ni matumaini yetu idadi yao itasaidia serikali kuwatambua na hatimaye nao kupata haki zao za msingi kama watoto wengine wanaopata malezi ya wazazi wao.

Kazi iliyofanywa na viongozi wa serikali za mitaa kuanzia wakati uhakiki hadi siku ya sensa imesaidia makarani kuwapata kwa urahisi watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kufanikisha zoezi hilo liende kama lilivyopangwa.

Elimu iliyotolewa imesaidia wananchi wengi kuelewa umuhimu wa kushiriki zoezi la kuhesabiwa kwa kuwa wanatambua bila serikali kujua idadi ya watu ilio nao haiwezi kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

Nia ni kuwezesha wananchi wote kufaidika na mipango ya maendeleo iliyowekwa na serikali kuanzia kwenye afya, elimu na huduma zote muhimu ikiwamo majengo bora.