Kutokana na umuhimu wa siku hii, Rais Samia Suluhu Hassan, alitangaza rasmi kuwa ni siku ya mapumziko ili kila mwananchi aweze kushiriki kuhesabiwa.
Serikali na wadau mbalimbali wamehamasisha wananchi kutoa ushirikiano wa kuhesabiwa ili iweze kujua idadi ya watu wake na mahitaji yao kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Maandalizi yote ya kufanikisha siku hiyo yamekwenda vizuri na tumeelezwa kuwa yamekamilika kwa asilimia 100.
Makarani wa sensa, wameshapangiwa vituo vyao vya kutembelea wananchi kwenye mitaa na makazi yao na kwa mujibu wa elimu waliyopatiwa, hawaruhusiwi kutoa siri za taarifa zitakazotolewa na wananchi.
Upungufu wowote uliojitokeza wakati wa maandalizi bila shaka umefanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi ili siku hiyo kusiwe na kisababishi chochote cha kukwamisha zoezi hilo.
Zoezi hili litahusisha ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa wananchi wote kwa maana ya wanawake na wanaume, watoto na watu wazima, wenye ulemavu na wasio na ulemavu. Na litafanyika pande zote mbili za Muungano kwa maana ya Tanzania Bara na Visiwani.
Takwimu zitakapopatikana katika zoezi la sensa zitasaidia kuboresha huduma mbalimbali za wananchi kuanzia sekta ya afya, elimu, maji, umeme na nyingine muhimu kwa jamii.
Kwa mfano, takwimu za sensa zitasaidia Wizara ya Afya katika kuandaa sera na mipango ya afya inayolingana na idadi ya watu katika eneo husika kwa kuzingatia mahitaji yao ya huduma hiyo. Mfano kwa kujua idadi na umri wa watoto nchini na hali zao za kiafya wizara itaweza kuandaa mpango wa kuagiza/kununua idadi na aina ya chanjo kuendana na idadi ya umri halisi wa watoto katika nchi nzima au wilaya husika. Wananchi pia waelewe kuwa mipango yote hupangwa kwa kutumia takwimu za sensa na pia utoaji huduma za afya huendana na takwimu zinazotokana na zoezi hilo. Mfano
ujenzi wa hospitali ya wilaya katika kata eneo husika huhitaji idadi ya wakazi wasiopungua 80,000. Takwimu za sensa pia zitasaidia Wizara ya Elimu kujua viwango vya elimu vya Watanzania wote na kuandaa sera na mipango ya elimu kulingana na idadi, viwango vya elimu na mahitaji ya kielimu ya watu katika eneo husika.
Wizara ya Elimu nchini ipo katika mchakato wa mabadiliko ya mitaala ya elimu ili kuendana maendeleo ya sayansi na teknolojia na mahitaji ya wakati uliopo. Takwimu hizi za sensa zitasaidia utekelezaji wa mchakato huo muhimu unaotegemewa kuleta mabadiliko na maendeleo makubwa katika sekta ya elimu nchini. Mfano kwa kujua idadi ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika, wizara inaweza kuandaa mpango maalumu kwa kuanzisha masomo ya watu wazima nchini ili kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kwenye jamii. Pia idadi kubwa ya watoto katika eneo husika itaonesha uhitaji wa kuongeza madarasa na walimu zaidi kulingana na idadi ya watoto iliyopo. Wananchi waelewe kuwa mipango na utoaji huduma za elimu nchini hufanywa kwa kuzingatia takwimu za sensa.
Hizo ni baadhi tu ya faida ya sensa katika kuandaa mipango ya maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kuelewa umuhimu wa kushiriki kuhesabiwa.









