Kwa wale walioitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, walianza kujiunga nacho jana wakati huu kalenda hiyo ya Fifa ikitarajiwa kudumu hadi Septemba 04, mwaka huu.
Kwa upande wa Taifa Stars, imeingia kambini kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Soka la Ndani (CHAN), zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Algeria.
Stars inatupa karata yake ya mwisho katika kinyang'anyiro hicho kwa kuvaana nyumbani na ugenini dhidi ya Uganda kati ya Agosti 26-28 na kurudiana kati ya Septemba 2-4, mwaka huu, na timu itakayopata matokeo ya jumla katika michezo hiyo miwili, itafuzu moja kwa moja fainali hizo.
Hata hivyo, kuwapo kwa kalenda hiyo ni wazi kutakuwa kumewatibulia wawakilishi wetu wa nchi kwenye maandalizi yao michuano klabu ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambayo mechi za awali zinatarajiwa kupigwa kati ya Septemba 9-11 kabla ya marudiano Septemba 16-18, mwaka huu.
Ikumbukwe kwa Tanzania Bara, Simba na Yanga ndizo zinazobeba jukumu la kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa wakati Azam FC na Geita Gold FC zikibeba dhamana ya kuipeperusha vema bendera ya nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, Azam FC yenyewe haitakuwa imeathiriwa sana na kalenda hiyo ya Fifa kutokana na ukweli kwamba itaanzia raundi ya kwanza, itakayopigwa Oktoba 7-9 na marudiano Oktoba 14-16, mwaka huu.
Hivyo, pamoja na ukweli kwamba wawakilishi wetu hao, makocha wataathirika katika programu zao za mazoezi kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji, bado wanapaswa kuendelea kuwanoa watakaobaki kwa kuwa tunaamini hata wale waliopo timu za taifa wanapata mazoezi ya kutosha na kitakachokosekana ni mbinu za pamoja kama kikosi.
Hii ni kutokana na wachezaji walioitwa tu kwa upande wa Taifa Stars ni saba kutoka Klabu ya Simba, Yanga (6), Azam (5) na watatu kwa Geita Gold, idadi ambayo inaweza kuongezeka kwa klabu hizo kama wachezaji wao wa kigeni wataitwa kwenda kuzitumikia nchi zao kwenye mechi za kirafiki.
Kwa mantiki hiyo, hadi kukamilika kwa Kalenda ya Fifa, zitakuwa zimebaki siku tano tu kabla ya wawakilishi hao wa nchi kimataifa kwa ngazi ya klabu, kuanza kurusha karata zao za kwanza kwa Simba kwenda nchini Malawi kuivaa Nyasa Big Bullets huku Yanga ikielekea Sudan Kusini kuvaana na Zalan FC na Geita Gold ikikwea pipa kuifuata Hilal Alsahil SC ya Sudan.
Hivyo, huu ni wakati kwa wawakilishi hao wa nchi kuendelea na maandalizi makubwa hasa ukizingatia pamoja na ligi kuanza na kuchezwa michezo miwili kwa kila timu, bado klabu hizo hazijapata muunganiko mzuri ambao unaweza kuleta matumaini ya kwenda kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Tunataka kuona zote zikifuzu kwa kishindo kuingia raundi ya kwanza na kisha kuvuka hadi hatua ya makundi kwenye michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika, na hilo linawezekana tu kama maandalizi yataendelea kufanyika kwa umakini mkubwa.
Lakini wakati huu ambao dirisha la usajili la Ligi Kuu Bara likiwa wazi, ni wakati sahihi kwa wawakilishi wetu hao kuziba panapovuja mapema kabla ya kuelekea katika michuano hiyo migumu na yenye ushindani mkubwa.
Tunaamini katika michezo hiyo miwili ambayo kila timu imecheza kwenye Ligi Kuu, inaweza kuonyesha mapengo ambayo yanatakiwa kuzibwa mapema kabla kuingia katika kinyang'anyiro hicho cha michuano ya CAF.
Hayo yakifanyika kwa umakini mkubwa, tunaamini wawakilishi wetu wataanza michuano hiyo kwa kishindo na kujenga matarajio makubwa kwa Watanzania kushuhudia wawakilishi wetu hao wakiweka historia kwa wote kutinga hatua ya makundi, jambo ambalo tunatamani kuliona likitokea kwa mara ya kwanza kwa nchi yetu kwenye michuano hiyo.









