Hapa nchini shughuli hiyo inafanyika katika sehemu mbalimbali mikoani kwa wadau kutoa elimu iwe kupitia warsha, semina na maonesho.
Watoto wanakumbana na changamoto mbalimbali katika jamii ikiwamo kufanyiwa vitendo vya ukatili, iwe majumbani, shuleni na hata katika maeneo wanayocheza.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi mbalimbali za kutetea haki za watoto, wengi hukumbana na changamoto hizo kutoka kwa ndugu zao wa karibu na baadhi ya wazazi pia uhusishwa na vitendo hivyo.
Siku hii ilianza kuadhimishwa tangu mwaka 1991 ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano mji wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 kupinga mauaji ya watoto wenzao na pia kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto.
Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika imekuwa ikiadhimisha siku hii tangu mwaka 1991. Lengo la kuadhimisha siku hii ni kukumbuka mauaji ya kinyama waliyofanyiwa watoto wa kitongoji cha Soweto.
Maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Maadhimisho haya yawe chachu kwa jamii kuwalinda watoto bila kujali kama umemzaa wewe. Kuna msemo unaosema mtoto wa mwenzako ni wa kwako hivyo, kila unapomuona mtoto akifanyiwa unyama au udhalilishaji na ukatili wa aina yoyote, wajibu wako ni kumnasua katika hali hiyo kwa kuripoti kwenye vyombo vinavyotakiwa ili hatua ichukuliwe mara moja.
Vitendo vya ukatili wa watoto vinaendelea kushamiri maeneo mbalimbali nchini kutokana na jamii kutolibeba jukumu la malezi kwa watoto hao. Mtoto akionekana anafanyiwa ukitili baadhi ya jamii huliacha bila kuchukua hatua na kusababisha waendelee kupata mateso na kukosa haki zao za msingi ikiwamo uhuru wa kuishi.
Watoto wengine wanakosa haki ya kupata elimu kwa sababu ya kutumikishwa kazi za nyumbani au kufanyiwa vitendo vya kinyama vya kutumikishwa kingono.
Kama jamii itajitwisha jukumu la maelezi bila kujali kwamba mtoto huyo sio wa kwako, tatizo la ukatili litapungua.
Hii itasaidia hata mtu anayetaka kumfanyia ukatili mtoto kuogopa kwa sababu atakuwa anajua kuna watu wanamwangalia. Kwa pamoja tukishikamana tatizo hili la ukatili wa watoto litatokomezwa.










