Taifa Stars ina mlima mrefu kufuzu Afcon

17Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taifa Stars ina mlima mrefu kufuzu Afcon

TIMU ya taifa, Taifa Stars, ilishindwa kupata ushindi kwenye mchezo wake wa pili wa kuwania kufuzu kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2023, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Stars ilipoteza mchezo huo baada ya awali kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Niger kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Cotonou, nchini Benin.

Matokeo dhidi ya Algeria siyo ya kushitua kutokana na kiwango chetu dhidi yao, lakini kwa kuzitazama dakika 90 za mechi hiyo ziliibua mshangao kwa namna mabao yalivyopatikana na mwisho kujikuta tumepoteza mechi.

Pamoja ya kufahamika ujanja walionao wachezaji wa Algeria, ambao wengi wao wanakipiga ligi za Ulaya, lakini Stars ilionesha kumudu angalau kasi na ujanja wao kwa kuuchezea na kujaribu kutafuta nafasi mbele yao.

Hata hivyo, juhudi zote hizo zilikwama kwenye sehemu ndogo ndogo mno zilizohusisha utimamu wa kumudu presha ya mchezo na mbinu chache, ambazo bado mpaka leo ni kikwazo kwenye kikosi hicho cha kocha Kim Poulsen.

Stars ilianza mechi hizi za kufuzu kwa morali kubwa baada ya kupata sare na Niger huku Uganda ikifungwa mabao 2-0 na Algeria.

Lakini sasa mambo yameanza kuwa magumu katika mechi ya pili tu. Mechi ijayo tutaumana na Uganda kwao kisha tutarudiana tena hapa kabla ya kucheza na Niger kisha kuifuata Algeria kwao.

Kimahesabu tunaona kwamba, ni mlima mrefu mno kwa kuwa sasa, mazingira yameshakuwa mepesi kwa Algeria na waliobaki wanawania nafasi moja.

Kuwania nafasi kama hiyo dhidi ya Uganda na Niger si kitu rahisi tena ndani ya mechi nne tu zilizobaki, bado tunahitaji kuongeza umakini kwenye makosa madogo madogo yanayotugharimu kiasi hiki.

Stars inapaswa kujiamini na kufahamu ushindani ni ushindani pasipo kuwa na busara zisizo na msingi wala kuzubaa hata kidogo. Kuna muda mpira unakupa matokeo kwa mbinu tu na si ujuaji wa kuuchezea mpira sana.

Tunachotakiwa kufanya ni kuongeza mbinu na umakini, wachezaji wajitambue wanapopewa majukumu, kujitoa na kucheza na kuzingatia bahati zinazotokea ndani ya dakika 90 ni suala la msingi pia.

Kilichopo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Stars inaimarika vizuri zaidi kwenye mazoezi ili mechi zinazokuja ziwe kwa ajili ya kutafuta ushindi tu na sio sare.

Ni wazi kwamba, sasa zimebaki timu tatu kwenye kundi letu ambazo zinagombea nafasi moja, hivyo kazi ni kubwa mno kwa Stars kuweza kuupanda mlima huu, lakini kila kitu kinawezekana, tukiamua na kujidhatiti kwa nguvu moja.

Sisi tunashauri kwamba, benchi la ufundi kwa sasa linatakiwa kukaa chini kufikiri na kutafakari hizi mechi zilizobaki za Stars inaingiaje uwanjani, kwani tukipoteza mchezo unaofuata ni wazi nafasi ya kufuzu itakuwa finyu mno kwetu.

Sasa kazi iliyopo mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha kwa namna yoyote ile angalau tupate ushindi kwenye mechi mbili kati ya nne zilizobaki huku tukiombea maumivu kwa wapinzani wetu waweze kupoteza kwenye mechi zao.

Hapo angalau tunaweza kuwa na uhakika wa kufuzu, kwani bila kujali matokeo ya wapizani wetu, tutakuwa tumejihakikishia pointi saba kibindoni ambazo kwa namna fulani zinaweza kutusaidia kufuzu kwenda kwenye Afcon ambapo itakuwa mara yetu ya tatu katika historia baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1980.

Wito wetu kwa sasa, wadau viongozi na wapenzi wote wa soka kuungana pamoja katika kuhakikisha kwamba, Stars inapata nafasi ya kufuzu Afcon ili kuweza kulitangaza soka letu kimataifa na kuendelea kunyanyuka kwenye orodha ya viwango vya ubora vya Shirikisho la mpira wa miguu duniani, FIFA.