Hiyo ni kwa kuzingatia waraka wa Rais namba moja wa mwaka 1998 kuhusu hatua za kubana matumizi ya serikali na waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma namba mbili wa mwaka 2021 kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina na stahili za magari kwa viongozi katika utumishi wa umma ili kubana matumizi.
Kama wengi walivyoiita ni bajeti iliyoleta kicheko kwa watu walio kwenye vipato cha chini na kuleta maumivu kwa wenye vipato vya juu.
Katika bajeti hiyo baadhi ya kodi zilizokuwa zikiwaumiza watu wa hali ya chini zimeondolewa, lakini kwa wenye uwezo kuongezewa kwenye maeneo mengine yakiwamo ya burudani.
Kwenye maeneo ambayo yameonekana kutumika kwa gharama kubwa, ilielezwa kuwa kwa sasa serikali inatumia zaidi ya Sh. bilioni 558.45 kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari, mafuta ya uendeshaji, ununuzi wa vipuri na matengenezo.
Ili kupunguza gharama hizo imeamua itaondoa utaratibu uliozoeleka wa madereva kutumika kusafiri barabarani na viongozi kwa njia ya anga kwa lengo ya kuyakuta magari kwenye mikoa wanayokwenda kutekeleza majukumu yao.
Imebaini katika utafiti wa siri uliofanyika kuwa kwa siku moja magari ya serikali yaliyotoka Dar es Salaam yalikuwa 132 na yaliyokuwa yanakwenda kwenye jiji hilo yakipishana kwenda Dodoma ni 76 na mengine nane yalikuwa yamepinduka hali inayosababisha gharama kubwa kwa upande wa mafuta, matengenezo na hata posho wanazolipwa madereva.
Katika kuokoa gharama hizo ambazo serikali ilikuwa ikipoteza zaidi ya Sh. bilioni 50, sasa itawakopesha magari watumishi wenye hadhi ya kuwa na gari la serikali wawe na magari yao, wafanye matengenezo, wanunue vipuri wenyewe na masuala ya mafuta yaangaliwe kwa utaratibu unaofaa.
Hatua hiyo imeelezwa itaokoa zaidi ya Sh. bilioni 500 ambazo zitaelekezwa kwenye ununuzi wa dawa na kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati, na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Utaratibu huo ni wa busara na hata uangalizi wa magari hayo utakuwa mzuri tofauti na anayelitumia bila kujua maumivu ya kulitengeneza linapoharibika.
Mara kwa mara tumekuwa tukishuhudia magari ya serikali yanavyotumika ndivyo sivyo na hata wengine kubebea mizigo ambayo mingine haifai kubebwa kwenye magari hayo.
Uchungu wa kitu unachokigharamia unakufanya ukitumie kwa uangalifu ili kuokoa gharama zitakazotumika kikiharibika.
Utaratibu huu ukitekelezeka kama serikali yenyewe ilivyoeleza itaokoa mabilioni ya fedha ambazo zitakwenda kutumika kwenye mambo muhimu ikiwamo ununuzi wa dawa na kuokoa maisha ya wananchi wasio na uwezo wa kujitibu.
Vilio vya wananchi kila siku ni ukosefu wa dawa muhimu hospitali, kukosekana kwa majisafi na salama katika baadhi ya maeneo na huduma nyingine zinazogusa maisha ya wananchi.










