Royal Tour itumike kupanua uwekezaji nchini

15Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Royal Tour itumike kupanua uwekezaji nchini

WINGI wa watalii wanaoingia nchini kwa sasa unaonyesha kuchangiwa na matokeo ya filamu ya Royal Tour na kulegezwa kwa masharti ya corona ambayo yamesaidia wageni kusafiri bila vikwazo vigumu.

Programu ya filamu ya Royal Tour ilizinduliwa Aprili, 2022 katika Jiji la New York na Jiji la Los Angeles nchini Marekani na kuendelea katika Jiji la Arusha, Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma.

Katika uzinduzi nchini Marekani, zaidi ya watu 6,000 walishiriki wakiwamo viongozi wa kitaifa wa majiji husika, watu maarufu, wawekezaji, wadau wa utalii na uhifadhi na wafanyabiashara mbalimbali.

Uzinduzi huo pia ulishirikisha vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vikiwamo; vituo vya televisheni na redio vya CBS, Fox News, NBC, YouTube na PBS - Amazon Prime video.

Kwa mujibu wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), mwishoni mwa Machi, mwaka huu, chama hicho kimepokea wageni zaidi ya watalii 300,000 kutoka Ulaya na 50,000 Marekani hali inayofanya hoteli zinazopokea na kulaza wageni kuelemewa.

Tunasema huu ni mwanzo mzuri wa matokeo ya filamu ya Royal Tour kuutangaza utalii wa Tanzania na kufanya watu wa mataifa mengine ya nje kuvutiwa kuja kuona vivutio vyetu.

Fursa hii itumike kuwekeza kwenye hoteli nyingi zaidi zitakazoweza kupokea wageni badala ya kuwapoteza kwa kukosa pa kuwaweka.

Pia wageni wa mataifa mengine kama Ufaransa, Italia, Dubai, Uturuki pamoja na Spain, wameanza kuingia nchini kwa wingi kushuhudia vivutio hivyo.

Kiuchumi, maliasili na malikale zimeendelea kuchangia katika kuingiza fedha za kigeni na Pato la Taifa (GDP) kupitia utalii, ajira, nishati, elimu, utafiti, utamaduni, burudani na tiba. Sekta ya Utalii huchangia takribani asilimia 25 ya fedha za kigeni na zaidi ya asilimia 17 katika Pato la Taifa.

Kutokana na juhudi za serikali za kuendeleza na kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii nchini, idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka katika nchi mbalimbali duniani imeongezeka kutoka 9,847 mwaka 1960 hadi kufikia watalii 1,527,230 mwaka 2019. Kadhalika, kumekuwapo na ongezeko la mapato yatokanayo na watalii, kwa mfano mwaka 1995 mapato yalikuwa Dola za Marekani milioni 259.44 na yaliendelea kuongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019 kabla ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Kutokana na serikali kukabliliana na ugonjwa wa UVIKO-19 idadi ya watalii imeanza kuongezeka kutoka watalii 620.867 mwaka 2020 hadi kufikia 716,169 Oktoba 2021. 

Juni 4, mwaka huu, kwa mara ya kwanza kampuni ya watalii duniani ya Eurowings Discovery ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ikiwa na watalii 130 waliokuja kutembelea vivutio mbalimbali kama Mlima Kilimanjaro, Zanzibar, Serengeti na Ngorongoro.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema kuja kwa ndege hiyo ni heshima na jambo muhimu kwa sekta ya utalii, huku Mwenyekiti wa Bodi ya KADCO, Dk. Natu Mwamba, akisema filamu hiyo imeongeza ujio wa watalii na wawekezaji nchini.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alilieleza Bunge kuwa kwa sasa kuna mafuriko ya watalii huku akisema mji wa Karatu umepokea wageni wengi kuliko miaka mingine na kichocheo kikubwa ni filamu ya Royal Tour.

Wizara ya Maliasili pia imeendelea kuhamasisha utalii wa ndani kupitia kampeni na programu mbalimbali, hatua ambazo zimeongeza idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi, vituo vya malikale na makumbusho kutoka watalii 562,549 mwaka 2020 hadi 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2. Ongezeko la idadi ya watalii limechangiwa na juhudi mbalimbali zikiwamo; kampeni za kutangaza utalii, maadhimisho na maonyesho mbalimbali.

Uhamasishaji huu uwe chachu pia ya kuboresha vituo vingi zaidi na kuvutia watalii wengi kuvitembelea.