Kwa kutaja machache tu miongoni mwa mambo aliyoyabainisha katika ukaguzi wake kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ni kasoro katika mkataba baina ya mamlaka hiyo na kampuni ya makontena ya TICTS, akisema umiliki wa asilimia 51 ya hisa wa TICTS ulihamishwa kwenda kwa kampuni ya Hutchison International Port Holding Desemba 30, 2005 kinyume cha matakwa ya mkataba na kuikosesha serikali mapato makubwa.
Aidha, alibaini Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inajiendesha kwa hasara, huku cheti cha uendeshaji wake kikiwa kimeisha muda wake tangu mwaka 2010.
Harufu ya fisadi imegundulika pia kwenye Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya kuzalisha umeme kwa gesi ya Songas, ambayo shirika hilo lina hisa na kusema katika mwaka wa fedha 2014/2015, Songas ililipa gawio la dola za Marekani milioni 3.9 kwa TPDC, lakini ukaguzi ulibaini kuwa Songas ilitangaza kulipa gawio la dola za Marekani milioni 15.
Alisema pia wamebaini udhaifu kwenye kurejeshwa mikopo inayotolewa na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), iliyotolewa chini ya mpango wa kusafirisha bidhaa nje kwa dhamana ya Serikali.
Ukaguzi huo umebainisha madudu mengi katika halmashauri kadhaa, ubinafsishaji wa UDA na katika taasisi nyingine ambazo hatukuzitaja hapa.
Pamoja na madudu hayo, ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa deni la taifa limekuwa kubwa na kwamba serikali imekuwa ikikopa ili kulilipa, hali aliyosema ni hatari kwa uchumi wa nchi.
Kwamba hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, deni la taifa lilikuwa Sh. trilioni 33.54, deni la ndani likiwa Sh. trilioni 7.99 na deni la nje Sh. trilioni 25.55, ikiwa ni ongezeko la Sh. trilioni 7.05 sawa na asilimia 27, ikilinganishwa na deni la Sh. trilioni 26.49 lililoripotiwa Juni 30, 2014.
Tunampongeza sana Assad na timu nzima ya ofisi yake kwa kazi nzuri iliyobainisha madudu mengi, kubwa zaidi ni kuonyesha kwamba hapajakuwapo nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Ripoti hiyo imesheheni mapendekezo mbalimbali kwa serikali kuhusiana na hatua za kuchukua kuziba mianya iliyoko ili fedha za umma zisiendelee kuliwa kama wafanyavyo mchwa na watu wachache waliopewa dhamana na umma.
Kwa miaka kadhaa, Ofisi ya CAG imekuwa ikiwasilisha ripoti za aina hiyo, lakini serikali inabaki kimya bila kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa, yakiwamo ya kuwaadabisha wahusika. Hii ndiyo sababu kubwa inayosababisha hali hiyo kuendelea kwa kasi.
Hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na ufisadi na kusisitiza nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, zinatupa matumaini kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi ikiwamo utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa bila kumlinda wala kumuonea mtu yeyote.
Ni matarajio yetu kwamba kuchukua hatua dhidi ya waliobainishwa kuhusika katika matumizi mabaya ya fedha za walipakodi kutasaidia kuwatia hofu watendaji wengine kutorudia vitendo hivyo, ambayo vinaendelea kuwaathiri Watanzania na kuishi katika lindi la umaskini.










