Muungano huo ambao uliasisiwa na waasisi wa nchi hizo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume, ni wa kipekee katika Afrika kutokana na kudumu kwa muda mrefu kulinganisha na nchi kadhaa zilizojaribu kuungana, lakini muungano wao haukudumu.
Miongoni mwa nchi zilizoungana, lakini muungano huo ulidumu kwa muda mfupi ni wa Senegal na Gambia ambazo ziliungana mwaka 1982, lakini mwaka huo huo muungano huo uliozaa taifa jipya la Senegambia, ulivunjika.
Sababu kubwa iliyotajwa kusababisha hali hiyo ni kwamba muungano huo haukutokana na matakwa ya watu, bali waliokuwa viongozi wa nchi hizo Abdou Diouf wa Senegal na Sir Dawda Jawara. Waliamua kuunganisha nchi zao baada ya Sir Jawara kupinduliwa na Jeshi akiwa ziarani Ulaya na Senegal kutuma wanajeshi wake na kufanikiwa kuzima jaribio hilo.
Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar sasa umedumu kwa miaka 52 ambao ni umri mkubwa wa binadamu, ingawa umekuwa ukikabiliwa na changamoto kadhaa kwa wakati wote wa uhai wake.
Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakisababisha changamoto ni mambo gani yawe ya muungano na yapi yasiwe ya muungano. Kwa upande mwingine suala la Zanzibar kudai mamlaka zaidi limekuwa likijitokeza mara nyingi na hadi sasa linaendelea kuibua mjadala.
Wakati wa mchakato wa katiba mpya mwaka 2013 awamu ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi na Bunge Maalum la Katiba lilipokutana mwaka 2014 mambo hayo yalionekana wazi wazi hususan suala la Zanzibar kutaka mamlaka zaidi. Baadhi ya wananchi hususan Wazanzibari wakati wa kutoa maoni yao walionekana dhahiri kuguswa na jambo hilo ikiwamo kuzungumza kwa hisia kali.
Huko nyuma Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ziliwahi kuunda timu ya pamoja kwa ajili ya kujadili kero za muungano na kuzipatia ufumbuzi, lakini baadaye timu hiyo haikuendelea na jukumu hilo.
Pamoja na kazi hiyo ya kuziainisha kero zote na kuzitafutia ufumbuzi kutokamilisha kazi yake, sisi tunadhani kuwa bado ipo fursa ya kuendelea na kazi hiyo kwa lengo la kuuboresha na kuudumisha muungano wetu uendelee kuimarika kwa manufaa ya watu wa pande zote.
Wakati kazi hiyo ikiendelea kufanyika, kuna haja pia ya wananchi wa pande zote kufanyia tathmini Muungano kwa kuangalia wametoka wapi, wako wapi na wanaelekea wapi wakiwa kwenye Muungano.
Ni wakati mwafaka kwa wananchi wa makundi yote kuujadili mafanikio na changamoto za Muungano kwa uwazi na bila woga. Pale panapoonekana kuhitaji maboresho basi yafanyike kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuuboresha na kuudumisha.
Ni matumaini yetu kuwa propaganda na vitisho kutoka kwa baadhi ya wahafidhina wasiotaka mjadala kuhusu Muungano havina tena nafasi kwa miaka ya sasa, bali kinachotakiwa ni hoja za msingi.
Tunawatakia Watanzania wote maadhimisho mema ya miaka 52 ya Muungano wetu, lakini tunawahimiza wauenzi kwa kuufanyia tathmini ya kina ili uende na wakati.










