Karibu maeneo yote ya Tanzania kipindi hiki yanapata mvua ambayo inatumiwa kwa ajili ya kilimo, lakini baadhi ya maeneo mvua hiyo imegeuka kuwa majanga kwa wakazi wake.
Mkoani Kilimanjaro, baadhi ya maeneo yameathirika kwa mfano, watu saba walifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku mali na mazao kuharibiwa katika wilaya za Moshi na Rombo kutokana na mvua kubwa zilizonyesha siku mbili mfululizo.
Nyumba na mashamba kadhaa katika wilaya hizo zilizingirwa na maji na serikali ya mkoa kuhitaji msaada wa helkopta kwa ajili kuokoa wakazi kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Kazi ya uokoaji ilikwama kwa muda kutokana na maji kuwa mengi, huku mkuu wa mkoa huo, Said Meck Sadiki, akitahadharisha kuwa kama mvua zitaendelea, yatatokea madhara makubwa zaidi.
Mvua hizo pia zilikata mawasiliano kati ya mji wa Bagamoyo, mkoani Pwani na eneo la Msata na kusababisha barabara hiyo kufungwa kutokana na mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko.
Eneo lingine kwa kutaja machache ni wilaya ya Kilosa, mkoani Morogor, ambako mvua zimekosesha makazi zaidi ya kaya 350 kutokana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko.
Walioathirika ni wakazi wa kijiji cha Mambegwa, kata ya Msowero, kutokana na nyumba zao kuanguka na nyingine kuzingirwa na maji na kupewa hifadhi ya muda katika Shule ya Msingi Mambegwa.
Hatuwezi kuyataja maeneo yote nchini ambayo yameathiriwa na yanaendelea kuathiriwa na mvua hizo, lakini tunashauri kuwa kinachotakiwa kufanyika ni kwa serikali na jamii nzima kuchukua hatua za haraka kuwasaidia waathirika.
Wote walioathirika kutokana na mvua hizo wanahitaji haraka makazi ya uhakika, chakula, dawa, maji, magodoro, mashuka na vifaa mbalimbali.
Msaada huo unahitajika haraka kwa kuwa bado mvua za masika zinaendelea kunyesha, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Mamlaka hiyo juzi ilitoa taarifa ikiwataka wananchi wa maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba kuchukua tahadhari kwani kuna uwezekano wa kunyesha mvua kubwa kuanzia juzi hadi kesho.
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa, utabiri wake unaonyesha kwamba mvua hizo zinatarajiwa kuambatana na upepo mkali unaozidi kasi ya kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili na uhakika wa kunyesha mvua hizo ni asilimia 80.
Huko nyuma watu walikuwa na mawazo kwamba mvua zinaathiri maeneo ya mabondeni tu, lakini ukweli ni kwamba mvua hizo zinaathiri hata maeneo yasiyo ya mabondeni.
Kwa kuwa serikali kila mwaka hutenga bajeti kwa ajili ya Kitengo cha Maafa kilichoko katika Ofisi ya Waziri Mkuu, sasa ni wakati mwafaka wa kuzitumia fedha hizo kuwasaidia wananchi wote ambao wameathiriwa na mvua ili warejee katika hali zao za kawaida.
Kupeleka misaada hiyo tunashauri kwende sambamba na ukarabati wa miundombinu iliyoharibika zikiwamo barabara, madaraja na njia za reli ili maeneo ambayo mawasiliano yakekatika yarejee katika hali ya kawaida na shughili ziendelee.










