Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kuchangia pato la taifa, serikali imekuwa ikijitahidi kutangaza vivutio vya utalii ambavyo vimezagaa karibu nchini kote ili kuwavutia watalii. Moja ya mikakati ya kutangaza utalii ambayo serikali imefanya ni filamu ya The Royal Tour aliyoicheza Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa gumzo katika sehemu mbalimbali duniani.
Sambamba na filamu hiyo, kumekuwa na juhudi kubwa za kutangaza vivutio vya utalii katika ukanda wa kusini vikiwamo vile vilivyoko katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kwa maana ya Iringa, Njombe, Rukwa, Mbeya na Katavi ambavyo vimekuwa havipati watalii wengi kama ilivyo vile vya ukanda wa kaskazini.
Matokeo ya filamu hiyo yameanza kuonekana baada ya juzi Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, kubainisha kuwa kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka huu, watalii 700,000 walitembelea vivutio mbalimbali vya utalii. Idadi hiyo ni ongezeko kubwa na la kujivunia kulinganisha na watalii 450,000 waliotembelea kipindi kama hicho mwaka jana.
Akizindua mkakati wa kutangaza utalii kusini mwa Tanzania katika hafla iliyofanyika mkoani Njombe, Waziri alisema idadi hiyo inatoa matumaini na kwamba bado watalii wanamiminika, hivyo kuwapo na nuru kwamba sekta hiyo imeanza kukua na kuchangia pato la taifa.
Pamoja na ujio huo mkubwa wa talii, bado kuna haja kubwa ya kuendelea kutangaza vivutio vya kusini mwa Tanzania ambavyo ni vingi vikiwamo hifadhi za taifa za Ruaha, Kitulo, Katavi na Udzungwa. Hifadhi hizo zina wanyama na ndege wa aina za kipekee, hivyo jitihada za kutangaza maeneo hayo zinaweza kuzaa matunda na nchi kunufaika na maliasili hizo.
Sambamba na hifadhi hizo, viko vivutio zaidi kama vile maporomoko ya Kalambo na Ngome ya Bismark mkoani Rukwa, Makumbusho ya Mkwawa Kalenga mkoani Iringa, Kaburi la Nyundo na Kimondo cha Mbozi. Pia katika mkoa wa Mtwara kuna eneo maarufu kama Shimo la Mungu ambalo pamoja na vivutio vingine hivyo, ni hazina kubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Ili kufikia azma ya kupata watalii wengi katika mikoa ya kusini, ni wajibu wa serikali na wadau wa utalii kushiriki kikamilifu kutangaza vivutio hivyo ikiwamo kutumia mitandao ya kijamii katika kuvitangaza. Kwa mantiki hiyo, kila mkoa uandae mpango kabambe ambao utawezesha kuutangza utalii ndani ya wilaya, mkoa na ukanda mzima.
Pia viongozi wa mikoa hiyo wanapaswa kuwahimiza wananchi wao kutembelea vivutio hivyo ili kujionea wanyama na vivutio vingine. Pongezi zinapaswa kumwendea Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo, ambaye hivi karibuni aliandaa ziara kwa watendaji wa kata na maofisa tarafa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuahidi kwenda kuwa mabalozi wa utalii kwa wananchi wao ili watembelee hali itakayokuza utalii.
Sambamba na mikoa na wilaya kuhamasisha utalii, jambo lingine la muhimu ni kwa wadau wa utalii hasa wamiliki wa hoteli na kampuni za kuongoza watalii, kuboresha huduma zao ili watalii wanapofika wasipate shida ya malazi na usafiri kwenda na kurudi kwenye hifadhi na maeneo mengine ya utalii.









