NEMC inapaswa kubadilika katika utendaji kazi wake

27Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
NEMC inapaswa kubadilika katika utendaji kazi wake

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limepewa dhamana kubwa katika kuhakikisha suala la mazingira nchini linasimamiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua dhidi ya watu, vikundi na taasisi zinazokiuka sheria zinazohusu mazingira.

Miongoni mwa shughuli muhimu za baraza hilo ni kutoa adhabu pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote na taasisi zinazovunja sheria, kanuni na taratibu kuhusu mazingira.

Kutokana na kupewa nguvu hizo kisheria, katika miaka ya karibuni jamii ilishuhudia viongozi wa NEMC, pamoja na mawaziri wenye dhamana ya masuala ya mazingira wakichukua hatua dhidi ya wakiukaji wa sheria ikiwamo kufunga baadhi ya viwanda vinavyochafua mazingira. Pia baraza hilo limekuwa likitoa matamko na maonyo mbalimbali dhidi ya wakiukaji wa sheria za mazingira.

Pamoja na kutekeleza majukumu hayo, hivi karibuni kumekuwa na malalamiko dhidi ya NEMC kuwa haitekelezi makujumu yake ipasavyo kubwa zaidi ikiwa ni ucheleweshaji wa vibali kuhusu tathmini na athari za mazingira. Vibali hivyo ndivyo vinavyotoa mwanga kwa wawekezaji na taasisi za serikali na za binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara, viwanda na masoko.

Mbali na ucheleweshaji wa vibali, NEMC pia imekuwa ikilalamikiwa kwa kutokuchukua hatua dhidi ya kampuni zinazojenga vituo vya mafuta karibu na makazi ya watu, jambo ambalo linadhaniwa kuwa kuna ukakasi katika kuruhusu utekelezaji wa kazi hizo.

Kadhalika, NEMC imekuwa ikilalamikiwa kushindwa kuwachukulia hatua wamiliki wa nyumba za starehe na ibada kutokana na kelele zinazotokana na muziki, hivyo kusababisha usumbufu kwa watu wanaoishi karibu na maeneo hayo.

Mifano halisi juu ya malalamiko hayo, kwanza ni kutoka mkoani Manyara ambako NEMC imelalamikiwa kwa urasimu wa upatikanaji vibali kwa wawekezaji wenye nia ya kuweka vitegauchumi mkoani humo. Mfano wa pili ni katika Manispaa ya Songea ambako baraza hilo lililalamikiwa kuchelewesha vibali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Kutokana na urasimu huo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere, amesema unakwamisha mkoa kupata wawekezaji hasa wa viwanda. Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba kwa mujibu wa Nyerere, kutokana na ucheleweshaji huo, mtu anaweza kukaa hata miaka miwili bila kupata kibali tangu alipowasilisha maombi katika ofisi za baraza hilo.

Athari za ucheleweshaji huo ni kubwa kwa kuwa miradi yoyote ile inatoa fursa za upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana ambalo ni tatizo kubwa hivi sasa. Sambamba na kukosekana kwa ajira, urasimu huo pia, unasababisha kudumaa kwa pato la taifa na uchumi wa wananchi.

Mwakilishi huyo wa Rais katika mkoa alishangazwa na hatua hiyo hata kuhoji labda NEMC ina kazi nyingi kiasi cha kushindwa kutoa vibali kwa wakati licha ya kuwa waombaji wanakuwa tayari wameshalipa ada mbalimbali kwa ajili ya upatikanaji wa hati hizo ambazo zinatoa mwanya kwa wawekezaji kuanza kutekeleza miradi yao.

Wahenga wanasema ngoma ikivuma sana mwishowe hupasuka. Kwa mantiki hiyo, NEMC inapaswa kuanzia sasa kujitafakari juu ya malalamiko na lawama inazotupiwa na kuchukua hatua ili kubadilika kiutendaji.