Hongera serikali kusaidia maandalizi Serengeti Girls

24Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hongera serikali kusaidia maandalizi Serengeti Girls

TIMU ya Soka ya Taifa ya Wasichana wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), inatarajia kuondoka nchini wikendi hii kuelekea Uingereza kuweka kambi maalumu ya wiki mbili kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Kombe la Dunia (U-17), zitakazofanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 30, mwaka huu huko India.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupeleka timu kushiriki fainali hizo za dunia na Serengeti Boys imepangwa Kundi D ikiwa pamoja na Canada, Japan na Ufaransa.

Katika kusaka tiketi ya kushiriki fainali hizo, Serengeti Girls inayofundishwa na Kocha Mkuu, Bakari Shime, ilianza kwa kuwaondoa yosso wenzao ndugu zao kutoka Afrika Mashariki na Kati Eritrea,  na Burundi na baadaye wawakilishi wa Afrika Magharibi, Cameroon.

Bara la Afrika linawakilishwa na mataifa matatu ambayo ni Nigeria, Morocco na Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Serengeti Girls imefika hatua hiyo baada ya kupambana na hii ilitokana na nguvu kubwa iliyoanza kuwekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo liko chini ya Rais, Wallace Karia ambaye aliahidi chini ya uongozi wake atahakikisha anatoa kipaumbele kwa soka la vijana na wanawake.

Hatimaye ndoto za Karia na viongozi wenzake zimetimia mwaka huu kwa kufikia malengo ya Watanzania kushiriki mashindano makubwa na kuacha kuwa watazamaji kama ilivyokuwa imezoeleka kwa kipindi kirefu.

Katika kuhakikisha timu hiyo inakwenda India kushindana na si kusindikiza wengine, serikali imegharamia safari ya Serengeti Girls kwenda Uingereza kujifua na hatimaye kuelekea kwenye michuano wakiwa imara.

Imeelezwa ikiwa katika mji wa Southampton huko Uingereza, timu hiyo itapata huduma za kiwango cha juu lakini pia itacheza michezo ya kirafiki kwa lengo la kuwajenga wachezaji na kuwaweka tayari kuelekea kwenye mapambano ambayo wametumwa na Watanzania wote.

Lakini mbali na kuisafirisha timu hiyo, serikali imewapatia jezi na vifaa mbalimbali vya mazoezi ili kuzifanya akili za wachezaji hao pamoja na viongozi wa benchi la ufundi wafikiri jambo moja tu la kusaka ushindi na kurejea nyumbani wakiwa mashujaa.

Nipashe linapenda kuipongeza serikali kwa uthubutu ambao imefanya wa kuhakikisha Serengeti Girls wanakwenda katika mashindano wakiwa hawana mawazo ya nje ya uwanja ambayo wakati fulani huchangia kushusha ubora na matokeo ya ndani ya dakika 90.

Tunawakumbusha wachezaji wa Serengeti Girls kuweka mbele uzalendo na kuhakikisha mnakwenda kupeperusha vyema bendera ya taifa na kuiweka Tanzania katika rekodi za juu na zenye heshima.

Ili yote yafanyike kwa ufanisi, wachezaji mnatakiwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja katika kipindi chote cha kuanzia kambini hadi kwenye mashindano, huu ni wakati muhimu sana kwenye maisha yenu lakini pia kwa Tanzania.

Mkumbuke mchezaji atakayefanya vyema kwenye fainali hizo, si tu ataisaidia nchi yake kurejea na taji, lakini pia atajiweka sokoni kwa klabu mbalimbali zitakazokuwa zinafuatilia wachezaji nyota kumsajili na hapo atakuwa amejifungulia milango ya kucheza soka la kulipwa.

Ili mafanikio haya yaliyopatikana yasionekane ni ya kubahatisha, TFF mnatakiwa kuendelea kuwekeza kwa wachezaji hawa vijana ambao baadaye watakapopandishwa kuchezea timu ya wakubwa (Twiga Stars), watakuwa wameiva na wenye uzoefu mkubwa na wataipa mataji Tanzania.

Hongera pia TFF kwa kuthubutu kuihudumia timu hii kwa zaidi ya miaka mitatu bila ya kuwa na wadhamini, matunda na juhudi za uwekezaji zimeonekana, tunaamini wakati umefika wa kukaa na wadhamini kwa ajili ya 'kuliuza soka la wanawake' kama ambavyo bidhaa nyingine (Liki Kuu Tanzania Bara), inavyotangazika.

Tunapenda kuwakumbusha wadau bado  Serengeti Girls inahitaji kudhaminiwa ili kuwa na mwendelezo wa kufanya vyema katika fainali hizi na mashindano mengine watakayoshiriki hapo mwakani ambayo yatahusisha timu ya umri chini ya miaka 20.

Wapo wadau mbalimbali walijitokeza kuisaidia Serengeti Girls na Tembo Warriors, tunawaomba msiishie hapo, wakati umefika mabosi wa kampuni na taasisi hizo wakaingia makubaliano ya udhamini na kwa kufanya hivyo si kutasaidia wawakilishi kufanya vizuri kwenye mashindano, lakini kutaongeza ajira kwa wote wanaoshiriki katika kusimamia timu hizo.