Kila mwananchi achukue tahadhari tishio la ebola

29Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kila mwananchi achukue tahadhari tishio la ebola

SERIKALI jana ilitangaza kuwa Tanzania iko kwenye tishio kubwa la kukumbwa na ugonjwa wa ebola ambao kwa miaka mingi umekuwa ikizisumbua nchi jirani ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Katika kutangaza tahadhari ya ugonjwa huo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliitaja  mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Mara na Kigoma kuwa kwenye hatari zaidi huku Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma kuwa katika hatari ya kati kutokana na mwingiliano wa viwanja vya ndege na vituo vya mabasi yanayotoka nchi jirani.

Akitangaza hatari hiyo, Waziri Ummy alisema ugonjwa huo haujaingia nchini lakini kuna hatari kubwa kupata kutokana na ukaribu wa eneo lililoathirika zaidi na ugonjwa huo wilayani Mubende, Uganda na mpaka wa Tanzania na Uganda wa Mutukula. Wilaya hiyo iko umbali wa kilomita 130 kutoka makao makuu ya nchi hiyo, Kampala.

Kadhalika, Kampala hadi Mutukula mkoani Kagera ni umbali wa kilomita 220 na kutoka Mubende kwenda Mutukula kupitia Masaka ni umbali wa kilomita 230, hivyo kuwapo kwa hatari kubwa ya kuwapo kwa ugonjwa huo kama tahadhari haitachukuliwa.

Licha ya umbali huo, ebola pia inaiweka Tanzania katika hatari kutokana na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia mipaka rasmi na isiyo rasmi. Watu wa Tanzania hasa walioko mipakani huvuka mipaka na kwenda nchi jirani sambamba na wa nchi hizo kuvuka mipaka na kuingia nchini. Hatari hiyo pia inatokana na kuwapo kwa wasafiri wa anga na nchi kavu kutoka na kuingia Tanzania.

Pamoja na kutoa tahadhari hiyo, Waziri Ummy alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwamo kupeleka timu ya wataalamu ya kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika mikoa iliyo kwenye hatari zaidi na maeneo yote ya mipakani.

Mbali na kupelekea timu ya wataalamu, serikali imewaagiza wakuu wa mikoa na viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa kuandaa mpango wa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo, kuimarisha ufuatiliaji na kutoa taarifa ya wahisiwa wenye dalili za ebola katika maeneo yao kupitia mfumo wa magonjwa ya mlipuko na yanayopewa kipaumbele (IDSR).

Serikali imeshatoa tahadhari juu ya tishio la ugonjwa huo ambao katika miaka kadhaa iliyopita, uligharimu maisha ya watu wengi hasa nchini DRC huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likiongoza kampeni ya kudhibiti tatizo hilo.

 Tishio la ebola linakuja huku Tanzania na dunia haijasahau madhara ya UVIKO- 19, ugonjwa ulioikumba dunia na kusababisha watu kupatwa na maradhi hayo pamoja na wengine kupoteza maisha. Kwa mantiki hiyo, jamii inapaswa kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kufuata taratibu zote za kujikinga.

Sambamba na kujikinga, hatua madhubuti zikiwamo kuwapima watu wanaoingia nchini kupitia vyombo vya usafiri hasa kwenye viwanja vya ndege na vituo vya mabasi. Pia ziandaliwe kambi maalum za kuwaweka watu watakaohisiwa au kujulikana kuwa na ugonjwa huo.

Aidha, kama ilivyo kuwa kwa UVIKO - 19, elimu ya afya kuhusu kujikinga na maradhi hayo inapaswa kutolewa kwa njia mbalimbali yakiwamo matangazo na picha za vikaragosi zinazoonyesha namna ya kujilinda na hatari hiyo.