Rushwa idhibitiwe katika uchaguzi viongozi wa CCM

30Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rushwa idhibitiwe katika uchaguzi viongozi wa CCM

HALMASHAURI Kuu ya CCM Taifa (NEC), juzi ilitangaza majina ya wagombea wa nafasi ya wenyeviti wa chama hicho ngazi ya wilaya katika uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii Tanzania nzima. 

Viongozi watakaochaguliwa katika kinyang’anyiro hicho, wataungana na wengine katika ngazi za mashina, matawi na kata kwa ajili ya kujenga chama hicho.

Kabla ya hatua hiyo, kulikuwa na sarakasi nyingi kuanzia kwenye ngazi za matawi  kiasi cha baadhi ya maeneo kutakiwa kurudia uchaguzi huo. Hata katika baadhi ya maeneo uchaguzi ulifutwa na kuagizwa mchakato kuanza upya.

Madai ya kuwapo kwa viongozi walioko madarakani kuwafanyia fitina wanaojitokeza kuwania na wengine kufutwa pamoja na kuwapo kwa tuhuma za rushwa zilitanda katika vyombo vya habari. Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya viongozi wakuu wa kitaifa katika ziara zao mikoani kukemea vikali na kuweka bayana kwamba watakaokiuka maadili watachukuliwa hatua.

Pia kukithiri kwa rafu hizo, kuliripotiwa kuwa zaidi ya wanachama  400 wa Kata ya Mahina, Nyamagana mkoani Mwanza, walitishia kurudisha kadi za uanachama kutokana na kasoro mbalimbali za uchaguzi wa mashina 80 na matawi manane. Huo ni mfano mmoja tu ni jinsi gani kulikuwa na rafu katika uchaguzi huo ngazi za awali kabla ya hatua ya wilaya.

Katika kutangaza majina ya walioteuliwa kugombea uenyekiti na nafasi zingine katika ngazi ya wilaya, kumekuwa na mabadiliko makubwa kutokana na baadhi ya waliokuwa wakishikilia nafasi hizo kuenguliwa. Hilo linajidhihirisha kwamba hatua dhidi ya baadhi ya waliojihusisha na ukiukwaji maadili zimechukuliwa.

Hiyo kwa kiasi kikubwa ni dhahiri kwamba inatokana na kauli aliyoitoa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, aliyesema wanafuatilia kwa karibu madai hayo na hatua zitachukuliwa kwa waliokiuka.

Ni imani kwamba chama kilipokea ripoti mbalimbali zilioeleza mazuri na kasoro, hivyo kuchukua hatua ikiwamo kuwaengua wale waliojihusisha na tuhuma za rushwa na upangaji wa safu za uongozi hasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwaka 2025.

Kwa kufanya hivyo, CCM inastahili pongezi na inaonyesha kuwa imedhamiria kwa vitendo kukomesha rushwa na ukiukwaji wa kanuni na maadili ya chama katika kupata viongozi bora kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.

Pamoja na pongezi hizo, ni vyema CCM ikafanya jitihada zaidi kuanzia sasa hasa kipindi hiki cha uchaguzi wa chama kuanzia ngazi ya wilaya kwa kuwa huko ndiko nguvu ya fedha inatumika zaidi. Kwa mantiki hiyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inapaswa kuongeza nguvu zaidi kuhakikisha uchaguzi unaoanza kesho hadi keshokutwa unafanyika kwa uhuru na haki.

Tunasema hivyo kwa sababu kama kutakuwa na rafu kwenye uchaguzi huo, ikiwamo watu kupata uongozi kwa njia za rushwa, kuna uwezekano mkubwa kwa chama hicho ambacho kimejijengea umaarufu ndani na nje ya nchi na kuwa na wafuasi wengi, kupata viongozi wabovu.        

Matokeo yake, uchaguzi huo unaweza kuibua mpasuko mzito ndani ya chama, hivyo kusababisha safari ya kuelekea 2025 kuwa ngumu katika baadhi ya majimbo, jambo ambalo litaigharimu CCM wakati huo ukifika.

Bado tunaamini kwamba CCM bado ni chama imara ndani ya Tanzania ndiyo maana imekuwa ikiaminiwa kila uchaguzi unapowadia na kupewa kura za kishindo kuendelea kushika dola. Sifa hiyo isiharibiwe na watu wachache hasa wanaotaka uongozi kwa kutumia fedha.