“Ulinganisho ni rahisi, kama tukilinda misitu yetu nayo itatulinda. Kama tukiharibu misitu yetu tunajiharibia wenyewe.” Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyoitoa Julai 2, nchini Suriname.
Kauli hiyo inatukumbusha kuwa binadamu na mimea tunategemeana kwa kiasi kikubwa, zaidi sisi binadamu tunaitegemea mimea kwa maisha yetu kuanzia kutupatia hewa safi, mvua na chakula.
Hata hivyo, binadamu wamekuwa waharibifu wakubwa wa misitu kwa kuikata na kusababisha nchi nyingi kugeuzwa majangwa na kilio cha mabadiliko ya tabianchi.
Nchi zinakosa mvua za kutosha kwasababu hakuna miti, upungufu wa chakula unatishia dunia kwasababu ya mabadiliko ya tabianchi na hali hii chanzo chake kinasababishwa na binadamu.
Ripoti mpya ya Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) iliyotolewa mwezi Machi, 2019 inasema majanga ya asili, ikiwamo mafuriko, vimbunga, joto la kupindukia, kuongezeka kwa kina cha bahari na matukio kama elnino, vyote vinaongezeka kutokana na mabadiliko haya ya tabianchi na hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa.
Hapa nchini mabadiliko ya tabianchi yameanza kuonekana kutokana na baadhi ya mikoa ambayo ilizoeleka katika kipindi fulani kuwa na mvua nyingi, sasa hivi zinakosa matokeo yanayosababisha kukosekana kwa chakula cha kutosha na tishio la njaa.
Elimu inatolewa mara kwa mara kuhusu athari za uharibifu wa mazingira zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi, lakini watu wanaohusishwa na uharibifu huo wameonekana kuziba masikio huku wakiendeleza hali hiyo.
Ukipita barabara inayoelekea Mkoa wa Pwani, unaweza kupigwa na butwaa jinsi wafanyabiashara wa mikaa wanavyojaza magunia kwenye malori na pikipiki kwa ajili ya kwenda kuuza mijini hasa Jiji la Dar es Salaam.
Ukipiga hesabu kwa siku si chini ya magari 10 na pikipiki 20 zinazosafirisha bidhaa hiyo ya mkaa kwenda mjini.
Ukiangalia idadi hiyo ya magunia utagundua jinsi gani misitu inavyoteketezwa na kuhatarisha nchi kugeuzwa jangwa.
Hali hii ya ukataji misitu inaathiri pia wanyama wanaotegemea chakula chao kutoka kwenye misitu hiyo.
Wafugaji wanalalamika mifugo yao kukosa chakula na kulazimika kuihamisha kutafuta sehemu zenye malisho ili isife njaa.
Baadhi ya wafugaji hao wamegeuka kuwa walinzi wa misitu isikatwe, lakini waharibifu hao wakigundua kuwa wanafuatiliwa, hugeuza muda wa kukata miti ambao hufanya mchana na sasa kukata usiku.
Wafugaji wanapopitisha mifugo yao kwa ajili ya kuwapa malisho hukuta tayari uharibifu umeshafanyika na kukosa njia nyingine ya kuwadhibiti.
Kama kungekuwa na ushirikiano wa kutoka kwa viongozi wa vijiji wa kudhibiti wahalifu hao, ukataji misitu ungedhibitiwa.
Lakini baadhi ya viongozi wanatuhumiwa kuhusika kuwaruhusu wahalifu hao kukata miti kwa kupokea kitu kidogo, bila kujali kuwa hali hiyo inaleta athari kubwa kwa nchi na vizazi vijavyo kwa nchi kugeuzwa jangwa.
Kwa pamoja wanaofanya biashara hiyo bila kibali cha mamlaka wakidhibitiwa na wengine wataogopa kwa sababu watajua sheria itachukua mkondo wake.










