Rais alikuwa akizindua majengo ya kutolea huduma ya afya ya uzazi hospitalini hapo.
Wakati akiteta na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa hospitali hiyo, Brenda Msangi, alimweleza kuwa wagonjwa wanaopokelewa miongoni mwao ni watoto.
Watoto kati ya miaka 12 au 11, hupokelewa wakiwa na fistula baada ya kubakwa, wanaofanya hivyo wanazalisha tatizo la maradhi.
Kiongozi huyo alisikitishwa jamii kufumbia macho tatizo la ubakaji kwa kutolisema na wanaotenda hawafikishwi kwenye vyombo vya sheria.
Alipotembelea wodini aliona mtoto wa miaka 12 na 13 ana ujauzito, ambaye hajui kitu kiasi cha kupata maradhi wakati wa kujifungua na wajawazito 12,000 hadi 19,000 wanaishi kwa tatizo hilo.
Alichokisema Rais ni tatizo halisi kwenye jamii kwa ambao wamejitokeza kufuata huduma za afya, lakini wapo waliofanyiwa ukatili kwa kulazimishwa kuolewa au kuolewa kwa ridhaa ya wazazi wao kwa kuwa sheria inaruhusu.
Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inaruhusu mtoto wa kuanzia miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au walezi wake, huku Katiba ya nchi ikitambua umri wa miaka 18 kama mtu mzima.
Mwanzoni mwa mwaka 2016, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, kupitia wakili Jebra Kambole, walifungua kesi kupinga kifungu cha 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa kinachoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 kwa kibali cha mahakama na ridhaa ya wazazi.
Aidha, Julai 8, mwaka 2016, Mahakama Kuu ilitoa hukumu ikikubali kwamba vifungu hivyo vya sheria ya ndoa vinapingana na Katiba ya nchi kwa kuweka umri tofauti wa kuoa na kuolewa kati ya mtoto wa kike na kiume.
Aidha, serikali ilisema inaangalia uwezekano wa kufanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kwa kushirikisha wadau wote muhimu.
Tunaungana na wanaharakati na wadau wengine juu ya umuhimu kwa kufanya marekebisho ya sheria hiyo, ili kuwaokoa watoto wa kike dhidi ya adha wanazopitia.
Katika umri wa miaka 14 bado viungo vya uzazi havijamudu mikikimikiki ya kubeba mimba na kulea mtoto, bali wanapaswa kuendelea kimasomo kwa nyanja mbalimbali.
Kutokana na sheria hiyo watoto wanakosa haki ya kusoma kwa baadhi ya jamii ambazo zinawaozesha wakiwa wadogo kwa kisingizio kuwa wamekubali, lakini kimsingi hawajakubali tamaa ya kupata mali.
Wengine wanaoolewa lakini bado hawajaweza kumudu mahitaji ya ndoa na kuhudumia familia, kwa kuwa ni jambo lenye kuhitaji mtu aliyekomaa kiakili.
Ni muhimu serikali ikaharakisha mchakato ili kuunga mkono jitihada za wadau ambao wanafanyakazi na jamii ngazi ya chini na wanaona tatizo lilivyo kubwa.
Kwa alichokishuhudia Rais jana ni jibu tosha kwamba kwenye jamii kuna tatizo kubwa ambalo linahitaji kushughulikiwa, ili kuwaokoa watoto wa kike wafikie ndoto zao.
Kuacha sheria hiyo kuendelea kutumika ni kichaka cha watu kuendelea kuwaumiza watoto wa kike kwa kuwalazimisha kuolewa na kuwaathiri kisaikolojia.










