Shule za kata zimeonyesha nuru ya mafanikio ya elimu

07Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shule za kata zimeonyesha nuru ya mafanikio ya elimu

BARAZA la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), juzi lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika Mei, mwaka huu. Matokeo hayo , yameonyesha kuwa  ufaulu wa jumla umeongezeka hadi kufikia asilimia 99.97 kulinganisha na asilimia 99.03 ya matokeo ya mwaka jana.

Licha ya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu, matokeo ya mwaka huu yametoa taswira nyingine baada ya shule mbili za kata kuwa katika orodha ya 10 bora na kuzibwaga shule kongwe za serikali na zile maarufu zinazomilikiwa na taasisi na watu binafsi.

Shule hizo, Mkindi ya Tanga na Ziba ya Tabora zimeshika nafasi ya tisa na ya 10  mtawalia zikiungana na Kemes (Kagera), Kisimiri (Arusha), Tabora Wavulana, AHMES (Pwani), Dareda (Manyara), Nyaishozi (Kagera) na Mzumbe ya Morogoro.

Hatua ya shule hizo kuchomoza katika nafasi 10 bora, ni ishara kwamba kumekuwa na maendeleo makubwa kitaaluma katika shule zilizoanzishwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) ulioasisiwa mwaka 2006. Kuasisiwa kwa mpango huo uliolenga kila kata kuwa na angalau shule moja ya sekondari, kulitokana na ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kutokana na mafanikio ya  Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).

Matokeo ya kwanza ya mitihani yaliyohusisha shule za MMES, maarufu kama shule za kata, yalionyesha shule nyingi kuburuza mkia na Watanzania wengi kubeza kwamba zilianzishwa kwa mtindo wa zimamoto. Baadhi ya wadau walidai kuwa kufeli kwa maelfu ya wanafunzi katika shule hizo, kulitokana na sababu mbalimbali zikiwamo uhaba wa miundombinu, ukosefu wa vitabu vya ziada na kiada, uhaba wa walimu, nyumba za walimu na hosteli.

Kutokana na matokeo hayo duni, serikali iliafiki kasoro hizo na kuweka mkazo katika kuzirekebisha kwa kuajiri walimu kila mwaka, kujenga vyumba vya madarasa,  matundu ya vyoo, maabara za masomo ya sayansi, nyumba za walimu na hosteli. Kero hizo zimekuwa zikipungua kila mwaka na hatimaye kiwango cha ufaulu kuanza kupanda mwaka hadi mwaka.

Kuibuka kwa shule hizo katika shule 10 bora ni dhahiri kwamba kiwango cha elimu katika shule zilizokuwa zikionekana hazina ubora, kumebadili fikra na mawazo yaliyokuwa yametawala, hivyo kuwa tishio kwa shule kongwe na maarufu zilizokuwa zikitamba mara kwa mara kila matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na cha sita yalipokuwa yanatangazwa.

Kwa hakika Mkindi na Ziba, ambazo ziko katika mazingira ya vijijini, zimeonyesha mfano na kuudhihirishia umma kwamba mpango wa serikali kuwa na shule katika kila kata ulikuwa na malengo mazuri ya muda mrefu katika maendeleo ya elimu.

Pia shule hizo zimedhihirisha kauli ya mara kwa mara ya serikali kwamba shule za kata miaka michache ijayo zitakuwa kimbilio kwa vijana wengi na hata kwa Watanzania waliokuwa na kasumba ya kuamini kwamba elimu nzuri inapatikana kwenye shule zinazomilikiwa na mashirika ya dini, taasisi na watu binafsi.

Kutokana na shule hizo kuibuka kidedea, ni nafasi ya shule zingine za kata kujifunza ni mbinu gani zilizotumika katika kuziwezesha kushika nafasi za juu za ufaulu ili kuongeza idadi ya shule za kundi hilo katika kupandisha kiwango cha ufaulu.

Pamoja na hayo, kama wahenga wasemavyo mgema akisifiwa tembo hulitia maji, walimu na wanafunzi wa shule hizo zilizozibwaga shule kongwe,  wasibweteke bali waongeze kasi na kuendelea kuwa katika kundi hilo pamoja na kuweka malengo ya kushika nafasi za juu zaidi.