Yanga walitawazwa kuwa mabingwa wa FA baada ya kuifunga Coastal kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-1, huku pia wao ndio wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu.
Kwa msimu huu kila timu ikivuna kile ilichopanda, lakini safari ya mavuno hayo ilikuwa ya kupanda na kushuka.
Simba baada ya kukosa ubingwa ilijihakikishia utawala wa nafasi ya pili na hakuna aliyekuwa akimsumbua hadi mwisho.
Presha kubwa ilianzia nafasi ya tatu hadi ya 15 na kuifanya ligi kunoga zaidi licha ya Yanga kutangaza ubingwa mapema.
Ukiacha Mbeya Kwanza ambao hawakusubiri mpaka mechi za mwisho na kushuka daraja mapema, timu nyingine zote zilizosalia zilibaki bila ya kujua hatima yao mpaka dakika 90 za michezo yao ya mwisho.
Azam ilifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu, ambapo ilihitaji matokeo ya ushindi pekee kwenye mechi ya mwisho bila kujali hatima ya Geita Gold iliyokuwa ikimfukuzia kwa karibu, lakini kama ingepata matokeo mengine, basi leo tungekuwa tunazungumza mengine.
Azam ilifanikiwa kuifumua Biashara United kwa mabao 4-1 na Geita kutoa sare ya 1-1 na Coastal Union na hivyo kuifanya Azam imalize kwa pointi 49 dhidi ya Geita waliofikisha 46. Kwa namna hiyo, Azam imeepuka kikombe cha kumsubiri mshindi wa fainali ya Kombe la FA ili ijue hatima yake ya ushiriki ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ni hivi, Yanga imeshakata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa ligi, na baada ya kuishinda Coastal maana yake, Geita iliyomaliza ya nne itakwenda Shirikisho Afrika.
Azam walionekana kupambana kumaliza nafasi ya tatu kwa udi na uvumba kiasi cha kuweka rekodi ya kuwa timu pekee msimu huu kushinda mechi nne mfululizo na sare moja katika mechi zake tano za mwisho za ligi.
Awali Azam ikiwa chini ya kocha George Lwandamina ilishindwa kusimama sawa sawa, ikitoka kwenye kuwania ubingwa na kuonekana ikitapatapa kwa matokeo yasiyoridhisha hadi ilipokabidhiwa kwa Abdihamid Moallin.
Moallin alianza kwa mbwembwe za ushindi kabla ya baadaye kupunguzwa spidi lakini akachanga karata zake sawa sawa na kurejea kwenye njia iliyompeleka kwenye mafanikio ya mechi za mwisho.
Kilichotokea kwa Azam mwanzo wa ligi ndicho kilichokuwa kwa Geita ambao ndio ulikuwa msimu wao wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara. Walianza vibaya chini ya Ettiene
Ndayiragije, wakamfurusha na mikoba akakabidhiwa Fred Minziro aliyeipandisha Ligi Kuu timu hiyo.
Minziro aakaibeba Geita, mara ya kwanza ilieleza malengo yake ni kusalia tu kwenye ligi lakini kwa mwendo aliokuwa nao wakabadili gia angani na kukomalia kumaliza nafasi nne za juu, mwisho imewezekana.
Geita pia ndiyo imetoa mfungaji bora msimu huu, George Mpole aliyefunga mara 17 dhidi ya Fiston Mayele wa Yanga waliyekuwa wakifukuzana kuishia kufunga mabao 16.
Namungo waliomaliza chini ya Geita, wao walikuwa na mwendo mzuri lakini ghafla mambo yalibadilika kwenye mechi za mwisho na hasa baada ya mshambuliaji wao namba moja, Reliants Lusajo aliposimama kufunga na kuganda mpaka mwisho wa ligi akiwa na bao zake 10.
Hata hivyo, uwepo wa David Molinga na Shiza Kichuya kwenye timu hiyo kulisaidia kuiweka kwenye ushindani wao wa awali, lakini ikajikuta inamaliza ya tano.
Hivyo kwetu sisi Nipashe tukiwa kama wadau wakubwa wa mpira wa miguu hapa nchini, tathmini yetu tunaona kwamba, kila timu imevuna kile ilichokipanda kwenye ligi hiyo.
Hata hivyo, tunaamini huu ni wakati muafaka kwa kila timu kujitathmini na kurekebisha upungufu uliyojitokeza na kujipanga vizuri sana kwa msimu ujao wa Ligi Kuu.Tunazitakia timu zote maandalizi mazuri.










