Kwa madudu haya ya posho, HESLB ijisafishe

02Sep 2016
Mhariri
Dar es salaam
Nipashe
Kwa madudu haya ya posho, HESLB ijisafishe

WAKATI serikali ikisisitiza nidhamu katika ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imebainika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kujilipa posho.

Hali hiyo imebainishwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuihoji HESLB sababu za kutumia Sh. bilioni 15.7 kulipana posho.

Baada ya kubaini matumizi hayo mabaya ya fedha za umma katika kikao cha juzi baina ya PAC na menejimenti ya bodi hiyo, baadhi ya wajumbe wa kamati walihoji ni kwa nini bodi hiyo isivunjwe na majukumu yake kutekelezwa na moja ya benki.

Huku wakionekana kuwa wakali, wakisema wakati wananchi wanaumia kutumia fedha nyingi kusomesha watoto wao, bodi yenye watumishi 144 pekee inatumia mabilioni ya fedha kufanya mambo yasiyo ya msingi.

Wabunge walikerwa na mlolongo wa posho zisizo za lazima ambazo wanalipana watumishi wa HESLB. Baadhi ya posho hizo ni iliyopewa jina la posho nyinginezo (other payroll allowance) ambayo mwaka ulioishia Juni 30, ilikuwa Sh. milioni 999.45 kutoka Sh. milioni 762.96 na nyingine inayoitwa posho maalum (special allowance) kwa mwaka 2015 ilikuwa Sh. milioni 582.05 kutoka Sh. milioni 463.96.

Kwa upande wa safari za ndani ya nchi, kwa mwaka 2015 Sh. milioni 979.5 zilitumiwa na bodi hiyo huku mwaka 2014 zikitumika Sh. milioni 665.09.

Safari za nje ya nchi kwa mwaka 2015 zilitumika Sh. milioni 697.38 na Sh. milioni 564.22 mwaka 2014.

Posho nyingine ni ya mahusiano na ukarimu (relationship and hospitality) ambayo kwa mwaka 2015 ilikuwa Sh. milioni 296.77 kutoka Sh. milioni 243.64 mwaka 2014.

Kuna madudu mengine mengi ya matumizi mabaya ya fedha ambayo pia yaliwashangaza wajumbe wa PAC, zikiwamo fedha za kikizo, maziko na rambirambi pamoja na matumizi ya bodi na ya manejimenti.

Kuwako kwa mlolongo wa posho hizo ambazo hazina tija, zaidi ya kuiingiza serikali hasara ni kiashiria kuwa fedha zilizokuwa zikipelekwa HESLB zilikuwa zinatumika kinyume cha lengo la kuwapatia mikopo wanafunzi wasio na uwezo wa kujilipia kusoma elimu ya juu.

Inaonekana kwamba viongozi wenye dhamana wakiwamo wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwaka jana wakati ule hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo na ndiyo maana fedha zilikuwa zinapelekwa HESLB na kutumika ovyo.

Sisi tuna imani na uongozi wa sasa wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambao umeshaanza kuchukua hatua kadhaa za kudhibiti ufisadi, ikiwamo kuwasimamisha kazi waliokuwa vigogo wa HESLB.

Uongozi wa sasa wa HESLB kwa maana na menejimenti na bodi unapaswa kutekeleza maelekezo ya nidhamu ya matumizi ya fedha za umma zikiwamo posho. Tunasema hivyo kwa kuwa menejimenti hiyo imekiri kwenye kikao na PAC kuhusu madudu hayo na kuahidi kurekebisha.

Tunaiunga mkono PAC kwa kuitaka HESLB kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na ulipaji wa posho uzingatie sheria na miongozo ya serikali.

Tunakubaliana na maoni ya wabunge kuwa kama HESLB itashindwa kusimamia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi na kubainika madudu mengine yatakayosababisha wanafunzi walengwa kukosa mikopo pamoja na matumizi makubwa ya fedha kulipana posho, ivunjwe na fedha zilipwe moja kwa moja kwa walengwa kupitia benki.