Tukio hilo limetokea mkoani huo ikiwa siku chache baada ya Shule ya Sekondari ya Mulbadaw wilayani Hanang’ kuungua kwa moto na kuteketeza mali za wanafunzi.
Moto katika Sekondari ya Aldersgate ulitokea usiku, wakati wanafunzi wanaoishi katika bweni hilo wakiwa madarasani kujisomea.
Taarifa za awali zilizotolewa na wanafunzi, walimu na walinzi, zilidai kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.
Matukio ya kuungua kwa mabweni yamekuwa yakitokea mfululizo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuanzia takribani miezi miwili iliyopita.
Katika mkoa wa Arusha takribani shule tano mabweni yake yaliungua mfululizo ndani ya mwezi mmoja. Hatuwezi kutaja majina ya shule zote, lakini baadhi ni Shule ya Sekondari ya Lowassa, Ole Sokoine, Longido na Erikisongo.
Mazingira ya moto huo yanatia shaka na kutoa picha kwamba inawezekana yanatokana na hujuma.
Kila tukio sababu zinazoelezwa na walimu, wanafunzi na walinzi ni hitilafu ya umeme, lakini swali linabaki ni je, kama chanzo ni hicho, ni kwa nini yaungue mabweni na siyo majengo mengine? Shaka nyingine ni mabweni ya baadhi ya shule yanaungua wakati shule hizo hazina umeme.
Kimsingi, picha halisi inayoonekana ni kwamba matukio ya kuungua kwa mabweni yanasababishwa na hujuma, ambazo haijulikani zinapangwa na kutekelezwa na nani na kwa lengo gani.
Ndiyo maana katika tukio la kuungua kwa mabweni katika Shule ya Sekondari ya Sokoine wilayani Monduli, Jeshi la Polisi liliwakamata na kuwahoji walimu wanne na wanafunzi wanane kutokana na kutajwa katika kura iliyofanyika kwa siri kwa ajili ya kuwabaini wahusika.
Viongozi wa Halmashauri ya Monduli walisema wanahisi kuwa matukio yaliyotokea wilayani humo ya kuungua kwa shule ni hujuma.
Kutokana na kasi ya matukio hayo, kuna haja kwa Serikali kuchukua hatua za haraka ikiwamo kuvitumia vyombo vyake kufanya uchunguzi wa kina utakaosaidia kuwabaini wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria.
Wadau kadhaa wakiwamo wabunge wa majimbo ambayo shule zake mabweni yameungua wamekuwa wakilalamikia matukio hayo na kuitaka Serikali kuchukua jitihada za makusudi ili kuyadhibiti kabla hayajaleta madhara makubwa zaidi.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imezungumzia matukio ya uchomaji moto katika shule na kusema yapo mambo mengi na kuahidi kuyatengenezea kitabu kitakachowasilishwa kwa wabunge ili wafahamu hali halisi.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bernard Makali, aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuwa kitabu hicho kitachapishwa na kukabidhiwa kwa waziri ambaye ataikabidhi kamati hiyo.
Kama ukweli umebainika, tunaona kwamba hatua za haraka zinahitaji kuchukuliwa kwa kuvikabidhi vyombo husika viufanyie kazi ukweli huo.
Tumaanini kuwa katika kikao kilichofanyika hivi karibuni cha maofisa elimu wa wilaya, sekondari, wenye shule za bweni na maofisa elimu wa shule zilizoungua pamoja na wakuu wa shule kilijadili suala hilo kwa mapana na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kudhibiti matukio hayo.










