Ligi Kuu ya Wanawake ifungue ukurasa mpya

03Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ligi Kuu ya Wanawake ifungue ukurasa mpya

KWA mara ya kwanza Tanzania inatarajia kuendesha Ligi Kuu ya Wanawake ambayo itaanza kwa kushirikisha klabu 10 kutoka mikoa mbalimbali ya Bara.

Kuanza kwa ligi hiyo ni hatua muhimu ambayo itafungua ukurasa mpya wa soka la wanawake ambalo bado lina safari ndefu kufikia kilele cha mafanikio.

Timu 10 ni ndogo, lakini si ndogo kwa kuanzia kwa sababu soka la wanawake limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali kuanzia kwenye ngazi ya klabu mpaka taifa.

Hakuna jambo ambalo litafanyika bia la kuwa na kasoro za aina yoyote, lakini hiyo isiwe sababu ya kulifanya jambo/ shindano/ au ligi hiyo kutofanyika kwa ufanisi.

Licha ya viongozi wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA) kutangaza ligi hiyo, lakini inajulikana wazi kuwa wasimamizi na waandaaji wakuu wa ligi hiyo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Tunapenda kuupongeza uongozi wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi kutimiza ndoto ya kuanzisha ligi ya wanawake, lakini pongezi hizi zitakuwa na maana pale tu ligi hiyo itakapofanyika kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.

Endapo kanuni na taratibu zitafuatwa, malengo ya kuhamasisha soka kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa yatafanikiwa na hapo soka la wanawake litacheza kila kona ya nchi yetu.

Mpira ni pesa, lakini mpira ni matokeo ya uwanjani, ligi hiyo ikichezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zake, hakuna shaka itavumbua vipaji mbalimbali ambavyo vitaisaidia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) kupata wachezaji wenye uwezo ambao wataipeperusha vizuri bendera ya nchi katika mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.

Tunatarajia Ligi Kuu ya Wanawake iwe na msisimko zaidi ya uliokuwa katika Ligi ya Wanawake iliyoendeshwa katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambayo ndiyo iliyozaa sehemu kubwa ya wachezaji wa Twiga Stars.

Ligi hiyo iliyokuwa chini ya Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (KIFA) ndiyo iliyobeba taswira la soka la wanawake hapa nchini na kuifanya mikoa mingine ianzishe michuano mbalimbali.

Kilichoonekana Kinondoni kilizaa matunda ambayo yalionekana kwa idadi kubwa ya wachezaji wake kuitwa katika kikosi cha Twiga Stars kilichokuwa chini ya Kocha Mkuu Boniface Mkwasa na hatimaye kukata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AWC) zilizofanyika mwaka 2010 huko Afrika Kusini.

Wakati TFF imejitahidi kuanzisha ligi hiyo licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa kukosa wadhamini, klabu zilizopata nafasi ya kushiriki zinatakiwa kuthamini uamuzi huo huku zikifahamu kwamba si wao peke yao ndiyo walistahili kucheza, ila taratibu ziliangaliwa na kuteua timu hizo.

Klabu zinatakiwa tumia vyema nafasi hiyo kwa kuhakikisha mshindi wa ligi anapatikana uwanjani na si kujipanga kukata rufani na kupata pointi za mezani.

Gazeti hili linaamini ligi hiyo ya wanawake itakuwa ni sehemu nyingine ya kushuhudia wachezaji wanakuza viwango vyao na hatimaye kupata nyota watakaosajiliwa na klabu za nje kama ilivyokuwa kwa Esther Chabruma kununuliwa Sweden huku Sophia Mwasikili alisajiliwa na klabu ya Uturuki.

Imeelezwa kabla ya kuanza kwa ligi, viongozi wa klabu teule watashiriki katika semina elekezi ambayo ni maalum kwa kupewa kanuni za ligi na taratibu nyingine muhimu.

Semina hiyo itumike vyema na viongozi wahusika ndiyo waruhusiwe kuhudhuria ili kuepushe sintofahamu wakati ligi hiyo itakapoanza.

Tunakubaliana na kauli iliyowahi kutolewa na Mkwasa kuwa endapo uwekezaji mzuri utafanyika katika soka la wanawake, Tanzania inaweza kupata nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake na hilo liko wazi kutokana na jitihada zinazoonyeshwa na wachezaji wanawake pale wanapowezeshwa.