Katika raundi ya kwanza kuna timu ambazo zilipata ushindi, nyingine zilitoka sare na zilizobakia zilipoteza pointi tatu muhimu kwenye michezo hiyo ya ufunguzi.
Majigambo na huzuni vimeonekana kutawala katika baadhi ya timu kutokana na matokeo ambayo wamepata kwenye mechi zao za ufunguzi ambazo zilimalizika Jumatano iliyopita.
Ni jambo la kawaida kwa timu iliyopata ushindi kuanza majigambo kwa kuamini iko katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa sababu iliondoka na pointi zote tatu muhimu.
Timu iliyoshinda inaamini kwamba ilifanya maandalizi sahihi kuanzia kwenye mchakato wa usajili hadi katika kucheza mechi za kirafiki na matokeo waliyopata wamestahili
Na kwa upande wa waliotoka sare, iwe ya mabao au ya bila kufungana, wanadhani kuna mahali ambapo walikosea na hicho ndio kimesababisha kukosa ushindi kwenye mchezo huo wa awali.
Lakini kwa timu zilizopoteza mechi zinaonekana kama hazikujiandaa vyema, hazikufanya usajili mzuri na wa kuzingatia mahitaji halisi huku zikionekana huenda pia zinafundishwa na makocha ambao hawana uwezo wa kushindana.
Nipashe tunawakumbusha viongozi na timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kukumbuka ndio kwanza kipenga kimelia, matokeo ya mechi za raundi ya kwanza yasiwafanye wakabweteka na kujisahau na maandalizi ya mechi zinazofuata.
Timu zinatakiwa kuendelea kujiandaa na kujiimarisha kwa ajili ya mechi zinazofuata na kuzingatia msimu huu ushindani umeongezeka kutokana na zawadi ya fedha zitakazotolewa na wadhamini waliopewa haki ya kuonyesha ligi hiyo kwenye televisheni, Kampuni ya Azam Media.
Tofauti na misimu iliyopita, Azam Media itatoa zawadi ya fedha mpaka kwa timu itakayonusurika kushuka daraja, hii ikiwa ni historia kwenye soka hapa Tanzania.
Lakini wachezaji nao wanatakiwa kujituma kwa ajili ya kutangaza vipaji vyao na kuwavutia makocha wa timu za taifa pamoja na mawakala kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Wakati wachezaji na viongozi wakifahamu vyema majukumu yao, waamuzi pia wanatakiwa kuhakikisha wanachezesha kwa haki mechi zote za ligi bila kujali timu au uwanja ambao anafanya kazi.
Mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu zinatarajiwa kuonyeshwa mubashara, hivyo wachezaji wanatakiwa kujituma na si kuchagua baadhi ya mechi, kubagua michezo hakumsaidii mchezaji au timu husika kwa sababu mechi zote zina umuhimu unaofanana.
Ni mapema mno kwa timu kukata tamaa kwa kuangalia matokeo ya mechi ya kwanza, ingawa pia timu hazitakiwi kubweteka kwa kusubiri michezo ya lala salama.
Ushauri huu pia unazihusu timu zote zinazotarajia kushiriki Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza), inayotarajia kuanza kesho, First League (Ligi Daraja la Pili), Ligi ya Mabingwa ya Mikoa na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Waswahili wanasema biashara asubuhi, jioni mahesabu. Usemi huu unazikumbusha timu na wachezaji wote kuamka mapema kwa kusaka pointi na hatimaye dakika za lala salama kuhakikisha wanakamilisha malengo na si kuwa kwenye nafasi za kujinusuru kuteremka daraja.










