Elimu ya uhamasishaji imekuwa ikitolewa na viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa dini, vyombo vya habari, wataalamu wa afya na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Semina zimekuwa zikitolewa katika maeneo mbalimbali na kuna wakati wahamasishaji wanawafuata wananchi kwenye maeneo ya mikusanyiko kama masoko, magulio na kwingineko.
Tunazipongeza jitihada zinazoendelea za uhamasishaji wa chanjo, lakini tunashauri kwamba ziendelee kubuniwa mbinu zaidi wa kwenda maeneo yenye watu wengi.
Kuna taarifa kwamba watu wa uhamasishaji wa chanjo hiyo mkoani Kigoma wameshauriwa kutumia vijiwe kama vya kahawa kwenda kutoa mada na kujibu maswali yanayowatatiza wananchi kuhusu chanjo.
Ushauri huo ulitolewa wakati wa kikao cha uhamasishaji wa masuala ya chanjo yaliyohusisha makundi mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari, viongozi wa dini, wafanyabiashara na makundi mengine.
Mmoja wa washiriki alisema uhamasishaji unaoendelea mkoani humo umekuwa ukiegemea zaidi maeneo ya barabarani pekee, lakini kuna fursa ya utoaji elimu ambayo bado hawajaifanyia kazi.
Alishauri ni vyema yakatumika maeneo yenye mikusanyiko ya kutosha na moja ya eneo hilo ni meza ya duara ambayo hutumiwa na wakazi wa Kigoma kujadili mada mbalimbali za kijamii, kisiasa na michezo.
Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma, Simon Chacha, alisema kila ushauri wenye tija wanaupokea na wanatarajia kufikia maeneo yote ili kuhakikisha kila mtu anapata elimu hiyo na majibu ya maswali yanayomtatiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi, Thobias Andengenye, alisema kuna haja ya kuyatumia makundi ya watu wanao hudumia watu wengi katika ufikishaji wa elimu hasa vijiweni.
Tunauona ushauri kwa wahamasishaji kwenda kutoa elimu vijiweni ambapo watu hukusanyika kwa wingi na pia ni maeneo yenye mijadala kuhusiana na mambo mbalimbali yanayotokea kwenye jamii.
Utaratibu wa wahamasishaji kusikiliza watu na kujibu maswali yanayowatatiza pia ni mzuri kama utatumika kwa sababu ni kweli kwamba kuna mambo mengine ambayo hawayaelewi vizuri kuhusu ugonjwa huo na umuhimu wa chanjo.
Pia upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu ni moja ya mambo ambayo wakati mwingine yanawatatiza wananchi, hivyo kwa kutumia utaratibu wa kujibu maswali ya wananchi, itasaidia kuwapa uelewa na kuona umuhimu wa kuchanja.
Ushauri wetu ni kwa serikali na wadau wengine kutoa sapoti ikiwamo kuwawezesha wahamasishaji ili wayafikie maeneo mengi yenye mikusanyiko mikubwa. Kwa upande mwingine, wahamasishaji wawe wabunifu kuhusu njia za kutumia katika kutoa elimu na kuhamasisha.










